Na Jimmy Kiango, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika ulimwengu wa burudani, umaarufu unaweza kumfanya msanii kuwa mali ya mashabiki kwa upande wa muziki, lakini maisha yake binafsi yakabaki kuwa eneo analohitaji kulilinda.
Hata hivyo, kwa nyota wa Bongo Fleva, Ali Kiba, maarufu kama Alikiba kati ya maisha ya kisanii na ya familia amewahi kuwa mwembamba, hasa katika kipindi cha misukosuko ya ndoa yake na Amina Khalef.
Ndoa yao ilianza kwa sherehe kubwa zilizofanyika Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania, Aprili, 2018.
Wakati huo, wawili hao walionekana kuwa miongoni mwa wanandoa waliovutia zaidi katika tasnia ya burudani Afrika Mashariki. Lakini nyuma ya picha za furaha, taarifa za kutokuelewana zilianza kujitokeza.
Mwaka 2022, Amina aliwasilisha ombi la talaka katika Mahakama ya Kadhi, Mombasa, akieleza kuwa ndoa yao ilikuwa imeharibika na kutaja changamoto mbalimbali za kifamilia.
Mwaka uliofuata, alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Alikiba kusaini nyaraka za talaka, akidai kuwa alikuwa ameshatoka katika uhusiano wao, lakini bado hakupata uhuru wa kuendelea na maisha yake.
Katika ujumbe wake wa Instagram Juni, 2023, Amina alidai kuwa Alikiba alikuwa akimzuia kupata talaka kwa kisingizio cha kulinda brandi yake.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa, huku mashabiki wakijiuliza, ikiwa umaarufu unaweza kuwa sababu ya kuchelewesha uamuzi muhimu wa maisha ya ndoa.
Alipokutana na waandishi wa habari, Alikiba aliulizwa kuhusu madai hayo na kwa nini, kwa mujibu wa Amina alikuwa akimkatalia talaka.
“Kiukweli hili suala ni suala binafsi. Naamini maisha yangu ya ndoa hayahusu kila mtu,” anasema akisisitiza kuwa masuala ya familia yake hayapaswi kuwa mjadala wa kila mtu.
Hata hivyo, alipokuwa akielezea changamoto za kuishi na mwenza, alitoa kauli iliyovuta hisia za wengi.
“Wanawake katika mwezi mmoja wana siku tano za kugombana na mwanamume. Wakimalizaga siku zao wanakuwa freshi,” anasema.
KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 10 – 16, 2026


