Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijiandaa kwa uchaguzi wa ndani wa mwaka 2027, majina ya viongozi watano yameanza kutajwa kuwania uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), nafasi inayoshikiliwa na Mohammed Ali Kawaida.
Harakati za chini kwa chini zimeanza ndani ya jumuiya hiyo, huku baadhi ya viongozi na makundi ya kisiasa wakipima nguvu na kujenga ushawishi kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuvuta ushindani kutokana na umuhimu wa UVCCM katika siasa za chama tawala, huku mijadala ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 ikitajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza joto.
UVCCM ina jukumu la kuhamasisha vijana kushiriki shughuli za chama, kutetea sera zake na kuibua hoja zinazogusa maendeleo ya vijana nchini.
Mjadala unaoendelea ndani ya jumuiya hiyo unahusu aina ya kiongozi anayeweza kuimarisha ushawishi wa CCM, wakati chama hicho kikikabiliwa na mijadala kuhusu Katiba Mpya, maridhiano ya kisiasa na matukio ya Oktoba 29, 2025.
Ingawa hakuna orodha rasmi ya wagombea, majina yanayotajwa katika mijadala ya kisiasa ni Rehema Sombi, Frank Nkya, Geofrey Kiliba, Ivan Moshi na Mwenyekiti wa sasa, Mohammed Kawaida.
Rehema Sombi
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi, anatajwa kutokana na uzoefu wake wa uongozi katika jumuiya hiyo na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Sombi amejenga mtandao wa kisiasa kupitia shughuli za chama na makundi mbalimbali ya kijamii, hususan wanawake na wajasiriamali.
Nafasi yake katika uongozi wa taifa inatajwa kumpa fursa ya kufahamika ndani ya jumuiya, ingawa bado haijulikani kama atajitosa rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho.
Miongoni mwa maswali yanayojadiliwa ni iwapo wajumbe watapendelea mwendelezo wa uongozi uliopo au kuchagua sura mpya.
Frank Nkya
Frank Nkya anaelezwa kuwa na uzoefu wa uongozi wa wanafunzi, utumishi wa umma na shughuli za Bunge.
Akiwa Chuo cha Ushirika Moshi, aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi na kushika nafasi ya uongozi katika Jumuiya ya Wazazi ya CCM, tawi la chuo.
Baadaye alihudumu kama Ofisa Tarafa Butiama na Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Pia amewahi kufanya kazi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Ofisa Sheria na Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
Kwa sasa anahusishwa na majukumu katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Nkya aliwahi kuwania uenyekiti wa UVCCM bila kufanikiwa. Hata hivyo, hajawahi kuongoza jumuiya hiyo katika ngazi ya wilaya au mkoa, jambo linaloweza kuwa changamoto katika kujenga mtandao wa wajumbe.
Geofrey Kiliba
Geofrey Kiliba, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), pia anatajwa katika mbio hizo.
Kiliba ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Asemewe Taifa, inayojihusisha na wanavyuo wanaounga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.
Uongozi wake katika taasisi za wanafunzi unatajwa kumpa nafasi ya kujenga ushawishi miongoni mwa vijana wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.
Hata hivyo, mtihani wake unaweza kuwa kupanua mtandao huo na kuwafikia wajumbe wa UVCCM nje ya mazingira ya vyuo.
Ivan Moshi
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi, ni jina jingine linalotajwa kuelekea uchaguzi huo.
Uzoefu wake wa kuongoza jumuiya katika ngazi ya mkoa unatajwa kumpa uelewa wa shughuli za UVCCM na mahitaji ya wanachama.
Moshi amekuwa akisisitiza amani, umoja na umuhimu wa vijana kuepuka kutumiwa katika migogoro ya kisiasa.
Changamoto inayotajwa kwake ni kujenga ushawishi mpana katika mikoa mingine, nje ya eneo ambalo amekuwa akifanya shughuli zake za kisiasa.
Mohammed Kawaida
Mwenyekiti wa sasa, Mohammed Ali Kawaida, naye anatajwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kuwania nafasi hiyo.
Kawaida alichaguliwa mwaka 2022, akichukua nafasi iliyoachwa na Kheri James baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya.
Kwa kuwa amehudumu muhula mmoja, baadhi ya wanachama wanaamini anaweza kuendelea kuongoza jumuiya hiyo iwapo ataamua kugombea tena.
Hata hivyo, Kawaida hajatangaza rasmi nia ya kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi ujao.
Walichosema wadau
Mchambuzi wa siasa, Seif Nassor, amesema UVCCM inahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kutatua changamoto za vijana badala ya kutegemea hotuba za kisiasa pekee.
“Kinachotakiwa ni kijana mwenye mwamko huo, kwa sababu chama kina matawi yake ya vijana, wazee na wanawake, hivyo yanatakiwa yatoe msaada wa kuizindua CCM na Serikali,” amesema.
Amesema mwenyekiti ajaye anapaswa kuwa na maarifa ya uongozi, biashara, uchumi na masuala ya kimataifa.
“Anatakiwa kijana mwenye taaluma ya uongozi, biashara na uchumi, kwa sababu uongozi wa sasa si kuongoza watu, bali unatatuaje changamoto zao?” amehoji.
Nassor amesisitiza umuhimu wa kupata kiongozi mwenye uwezo wa kuwaunganisha vijana bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa.
“Anatakiwa mwenyekiti atakayeizindua serikali na chama katika suala la maendeleo, hasa kuhakikisha ajira zinapatikana,” amesema.
Pamoja na majina hayo kutajwa, mchakato rasmi wa uchaguzi bado haujaanza na hakuna uthibitisho kwamba wote watawania nafasi hiyo.



