Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limerekodi mafanikio katika uhifadhi na kukuza utalii katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, likiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wanyama adimu, kuimarika kwa mifumo ya ulinzi na kupanuka kwa fursa za uwekezaji.

Mafanikio hayo yamepatikana wakati shirika hilo likikabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwamo ujangili, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2026, katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massina Mwishawa, amesema katika kipindi hicho shirika limeimarisha operesheni za kudhibiti ujangili na shughuli nyingine zinazokiuka sheria za hifadhi.

Amesema kati ya doria 314,940 zilizokuwa zimepangwa, shirika limefanikiwa kutekeleza 301,314, ambazo zimesaidia kuwakamata watuhumiwa 30,559 wanaohusishwa na matukio 25,006 ya ujangili.

Katika hatua nyingine, amesema operesheni hizo zimewezesha kukamatwa kwa mifugo 65,860 iliyokuwa ikiingizwa ndani ya hifadhi kinyume cha sheria, silaha 105 pamoja na kuondolewa kwa mitego ya nyaya 10,971 iliyokuwa ikitumika kuwakamata wanyamapori.

Mwishawa amesema mafanikio ya uhifadhi pia yanaonekana katika ongezeko la wanyama adimu, ambapo idadi ya faru imepanda kutoka 128 mwaka 2021 hadi kufikia wastani wa 170 mwaka 2026.

Aidha, idadi ya sokwe waliozoeshwa imeongezeka kutoka 196 hadi 288, huku mbwa mwitu 25 wakiachiliwa katika maeneo yao ya asili, ikilinganishwa na 12 waliokuwepo awali katika eneo la uzalishaji la Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Amesema katika kuboresha ulinzi wa hifadhi, Serikali imewezesha upatikanaji wa ndege nyuki 40 zitakazotumika katika doria za anga, sambamba na ujenzi wa vituo vitatu vya mawasiliano na minara 10 ya redio.

Kwa mujibu wa Mwishawa, matumizi ya teknolojia hiyo yameimarisha ufuatiliaji wa makundi ya tembo na kusaidia kuzuia matukio 9,787 ambayo yangeweza kusababisha madhara kwa wananchi.

Katika sekta ya utalii, amesema TANAPA imepanua wigo wa shughuli zinazoweza kufanywa na wageni ndani ya hifadhi kwa kuanzisha utalii wa puto, kutazama faru, utalii wa farasi, uvuvi wa kitalii, kuangalia nyota na safari za ndege za kutazama mandhari.

Pia, shirika limekamilisha ujenzi wa malango sita ya kuingilia wageni katika hifadhi mbalimbali na kuzindua uwanja wa gofu katika eneo la Fort Ikoma, lililopo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kuhusu uwekezaji wa malazi, amesema idadi ya vitanda katika loji na kambi imeongezeka kutoka 5,755 mwaka 2021 hadi 12,094 mwaka 2026, huku maeneo mapya 160 yakitengwa kwa ajili ya uwekezaji wa utalii, yakiwamo loji 30 na kambi 130.

Mbali na mafanikio ya uhifadhi na utalii, TANAPA imeendelea kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa zahanati tatu, nyumba mbili za waganga, vyumba viwili vya madarasa, bweni la wasichana na nyumba ya mwalimu, pamoja na kuweka mizinga 2,590 ya nyuki kwa ajili ya kukuza shughuli za ufugaji nyuki.

Vilevile, shirika hilo limewapatia mafunzo askari wa vijiji 410 kutoka vijiji 40 ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori.

Pamoja na hatua hizo, Mwishawa amesema shirika bado linakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji mikakati endelevu, ikiwamo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, mifugo kuingizwa hifadhini, kuenea kwa mimea vamizi na upungufu wa maji wakati wa kiangazi.

Changamoto nyingine ni kuendelea kwa vitendo vya ujangili pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko ndani ya hifadhi.

Akizungumzia hatua za kukabiliana na hali hiyo, amesema TANAPA imepanga kuongeza wigo wa doria, kushirikiana na vijiji katika kupanga matumizi bora ya ardhi na kuondoa mimea vamizi kwa kutumia mbinu za kisayansi.

Pia, shirika linatarajia kujenga mabwawa na visima virefu vitakavyosaidia kuhakikisha wanyamapori wanapata maji, hasa katika kipindi cha kiangazi.

Mikakati mingine ni kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia, kuboresha barabara na viwanja vya ndege, kuongeza vituo vya askari pamoja na kujenga vizimba maalumu vya kuzuia mamba na viboko.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji kuongeza uwekezaji katika hifadhi zilizopo Kanda ya Kusini, Mashariki na Magharibi, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza shughuli za utalii na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.