Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Dar es salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imekamata madumu 510 ya mafuta ya kula yenye ujazo wa lita 20 kila moja, yaliyokuwa yameingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia Bandari ya Kunduchi, Dar es Salaam.
Aidha, kupitia hatua zilizochukuliwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya Sh37,120,799 ikiwa ni ushuru na adhabu iliyolipwa kutokana na uingizaji wa bidhaa hizo bila kufuata taratibu za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 11, 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU, Elizabeth Mokiwa, amesema taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji katika eneo la Kunduchi na kufanikiwa kulikamata gari lililokuwa likisafirisha shehena hiyo ya mafuta.
“Tulifanya ufuatiliaji katika eneo la Kunduchi na kukamata gari lililokuwa limesafirisha shehena hiyo. Uchunguzi ulibaini kuwa mwagizaji wa mafuta hakuwa na nyaraka halali za uingizaji wa bidhaa nchini wala uthibitisho wa kulipa kodi na ushuru stahiki,” amesema Mokiwa.
Ameongeza kuwa baada ya kubaini ukiukwaji huo, TAKUKURU kwa kushirikiana na TRA ilichukua hatua za kisheria dhidi ya mwagizaji wa mafuta hayo pamoja na mmiliki wa gari lililotumika kusafirisha bidhaa hizo.
Kutokana na hatua hizo, jumla ya Sh37,120,799 zililipwa kama ushuru na adhabu, hatua iliyowezesha kurejesha mapato ya Serikali yaliyokuwa yamekwepwa kupitia uingizaji wa bidhaa hizo kinyume cha sheria.



