Na Mwandishi Wetu

WATUMISHI wa umma wametakiwa kujipanga kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi ya Akili Unde (AI), kwa kuyachukulia kama fursa ya kuboresha usimamizi na kukuza rasilimali watu katika taasisi mbalimbali.


Wito huo umetolewa na Ridhiwani Kikwete wakati akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu Afrika uliofanyika Novemba 10, 2026, katika Hoteli ya Verde, Zanzibar.

Mkutano huo uliofunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, uliwakutanisha takribani washiriki 1,220 wakiwemo Maafisa Tawala na Rasilimali Watu kutoka maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kikwete, mabadiliko ya teknolojia yanapaswa kuchukuliwa kama chachu ya kuimarisha usimamizi na ukuaji wa rasilimali watu badala ya kuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi.

Alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kujiandaa na mabadiliko hayo ili kuhakikisha teknolojia inatumika kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika taasisi zao.

Mkutano huo umejikita katika kujadili nafasi ya utumishi na ulinzi wa rasilimali watu katika kipindi hiki cha mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi yanayoongezeka ya Akili Unde.