Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema umuhimu na mafanikio ya sekta ya madini yametokana na juhudi za Serikali katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za madini, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuvutia uwekezaji, kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za madini.

Mkutano wa Uwekezaji wa Sekta ya Madini mwaka 2026 ni wa saba kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.

Mkutano huo ni fursa ya kuelezea manufaa muhimu yaliyopatikana katika sekta ya madini na utaendeshwa kwa kaulimbiu isemayo, “Madini yaliyoongezwa thamani: Chachu ya ukuaji wa viwanda na uchumi.”

Ameyasema hayo leo, Novemba 17, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, unaotarajiwa kufanyika Novemba 19 hadi 21, mwaka 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuhudhuriwa na washirikia 1700 kutoka ndani na nje ya nchi na makampuni mabalimbali ya madini

“Ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali kwenye sekta ya madini umeongezeka kutoka shilingi bilioni 884.09 kwa mwaka 2010 hadi trilioni 5.2 kwa mwaka 2025. Ongezeko hilo limetokana na usimamizi thabiti wa sera ya ushirikishwaji wa Watanzania,” amesema Waziri Mavunde.

Waziri amebainisha kuwa sekta ya madini ina mchango mkubwa katika Pato la Taifa, ambao umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo mwaka 2025 uliongezeka kwa asilimia 10.3 kutoka asilimia 7.8 ya mwaka 2024.

Hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa mauzo ya madini nje ya nchi. Thamani ya madini yaliyouzwa nje ya nchi iliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi Dola za Marekani bilioni 5.46 mwaka 2025.

“Kuongezeka kwa mapato ya Serikali. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, mapato ya Serikali kutoka sekta ya madini yalikuwa takriban shilingi bilioni 526. Kiasi hicho kiliongezeka na kufikia shilingi trilioni 1.39 katika mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Waziri Mavunde.

Hata hivyo, ushiriki wa Tanzania katika utoaji wa huduma na bidhaa katika shughuli za madini nchini umeongezeka. Ajira rasmi katika sekta hii zimeongezeka katika kipindi cha miaka hii, ambapo ajira rasmi zilifikia 10,874 kufikia Aprili mwaka 2025, huku asilimia 97.4 ya ajira hizo zikiwa ni za Watanzania.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye atakayefungua mkutano huo tarehe 19 Novemba mwaka 2026, na mkutano huo utafungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Pia kutakuwa na hafla ya Usiku wa Madini, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.