Wafanyabiashara wa Chakula na Vipodozi katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kuzingatia matakwa ya Viwango ili kulinda Afya ya watumiaji.
Rai hiyo imetolewa Leo na Katibu Tawala Wilaya ya Kahama Bi. Glory Absalum, wakati akizungumza katika Hafla ya Ufunguzi wa Viwango Clinic inayoendeshwa na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) kwa Wilaya ya Kahama akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Francis Daud.
Bi.Absalum amewasisitiza Wafanyabiashara kuhakikisha Wanasajili bidhaa na majengo ya Chakula na Vipodozi ikiwa ni pamoja na kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwa kumujibu wa Sheria.
Kwa upande wake Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Magharibi Bw.Joseph Makene, amesema Clinic hiyo ni fursa kwa Wananchi kukutana na Wataalam wa TBS kupata huduma mbalimbali zinazohusiana na Shirika hilo kwani TBS imewasogezea huduma karibu.
Baadhi ya Wafanyabiashara wakizungumza wamesema ni muhimu biashara zikafanyika kwa kuzingatia Viwango ili kuepuka athari kwa mlaji na Mtumiaji.
Viwango Clinic imeanza tarehe 16 hadi 20 Novemba 2026, ambapo Wafanyabiashara na Wananchi Wilayani Kahama wanapata huduma mbalimbali ikiwemo uthibitishaji ubora wa bidhaa,usajili wa bidhaa na Majengo ya Chakula na Vipodozi na Elimu ya Majukumu ya TBS kwa wananchi na wadau mbalimbali.


