Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar es Salaam
Serikali imesema uwekezaji katika sekta ya afya umewezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa takribani asilimia 80, huku vifo vya watoto vikishuka kwa asilimia 36, ikiwa ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto nchini.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Novemba 23, 2026, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Makuwani, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali, katika miundombinu ikiwemo kununua vifaa tiba ujenzi wa wodi za mama na mtoto na kuongeza madaktari bingww bobezi
“Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mafanikio haya yamechangiwa pia na utekelezaji wa Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyozinduliwa mwaka 2018 na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais, pamoja na mkataba wa kuimarisha lishe uliosainiwa mwaka 2022 kati ya Rais na wakuu wa mikoa.”amesema Dkt Makuwani
Hata hivyo amesema utekelezaji wa mikataba hiyo umeongeza upatikanaji wa dawa za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa zaidi ya asilimia 85 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku bajeti ya sekta ya afya ikiongezeka kutoka Sh trilioni 2.46 mwaka 2023/24 hadi Sh trilioni 3.7 kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Pia , amesema idadi ya zahanati imeongezeka kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067 na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194 katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2024/25, hatua iliyowezesha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilometa tano.
Katika hatua nyingine, amesema idadi ya magari ya kubebea wagonjwa imeongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka 2026, huku wodi maalumu za watoto wachanga zikiongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025.
“Mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama umewezesha kusafirisha wagonjwa wa dharura 250,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020 hadi Agosti 2026, ambapo asilimia 81 ni akina mama, asilimia 18 watoto wachanga na asilimia moja ni mama na mtoto kwa pamoja.”amesema Dkt Makiwani
Kuhusu huduma zinazotolewa, Dkt. Makuwani amesema kiwango cha wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza kimeongezeka hadi asilimia 86 kutoka asilimia 84 mwaka 2022, huku wanaohudhuria kliniki angalau mara nne wakiongezeka kutoka asilimia 65 hadi 81.
Amesema pia kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kimeongezeka kutoka asilimia 81 mwaka 2022 hadi asilimia 85. hivyo Serikali inaendelea kuimarisha huduma za watoto wachanga, ambapo watoto 91,000 walipatiwa huduma katika wodi maalumu za watoto wachanga katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2026, ikilinganishwa na watoto 71,000 waliohudumiwa mwaka 2025.
Dkt. Makuwani amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambuliwa katika ngazi ya Afrika na kimataifa katika kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, huku Rais Samia akitunukiwa tuzo ya Goalkeepers Award ya Gates Foundation Februari 2025 na kutambuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika huduma za mama na mtoto.
Aidha amesema hatua inayofuata ni kuendeleza mafanikio hayo kupitia Mkutano wa Tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Lishe utakaofanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, ulioandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na wadau wa maendeleo.
Ameeleza kuwa mkutano huo utajadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano hadi chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wachanga hadi chini ya 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030.
Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo, ambapo pamoja na kufungua mkutano, atashuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Pili wa Uwajibikaji kwa Wakuu wa Mikoa, kuzindua ripoti ya hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini pamoja na kuwakabidhi wakuu wa mikoa Mpango wa Nne wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto.









