Na Ssgt Mawazo Mtondo na Wdr Seif Baruti – Kilimanjaro
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Paschal Katambi, leo Novemba 25, 2026, amesisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Magereza, sekta binafsi na taasisi za serikali ili kuwapa wafungwa fursa za ajira na kutumia ujuzi walioupata wakiwa gerezani mara baada ya kumaliza vifungo vyao.
Waziri Katambi ameyasema hayo katika hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano kati ya Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), akisisitiza kuwa makubaliano hayo yasibaki kuwa nyaraka za kuwekwa kabatini, bali yatekelezwe kwa vitendo na kufanyiwa ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP. Jeremiah Yoram Katungu, amesema wafungwa 481 waliokidhi vigezo baada ya tathmini wanatunukiwa vyeti vya kurasimisha ujuzi walioupata kupitia mafunzo ya vitendo walioupata kupitia Jeshi la Magereza.
Amesema hafla hiyo ni mwendelezo wa utaratibu ulioanza mwaka 2024 mkoani Morogoro, ambapo wafungwa 201 walitunukiwa vyeti, huku ushirikiano huo ukiweka msingi rasmi wa mafunzo na urasimishaji wa ujuzi kwa wafungwa.
Aidha, CGP Katungu amesema Jeshi linaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais ya Mei 9, 2026, ikiwemo kuboresha programu za urekebishaji, kuandaa Mfuko Maalum wa kuwasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo( start-up kit) na utaratibu wa Bima ya Afya kwa wafungwa. Pia, utafiti wa kiwango cha wafungwa kurejea kwenye uhalifu umekamilika na Mfumo wa Taarifa za Wafungwa (PIMIS) umewekwa katika magereza nane.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Daniel Mushi, amesema hafla hiyo inaashiria hatua mbili muhimu, kutunukiwa vyeti kwa wafungwa 481 kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi pamoja na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya kimkakati kati ya VETA na Jeshi la Magereza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kupitia Mpango wa Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi (RPL), wafungwa 695 wamerasimishiwa ujuzi wao tangu mwaka 2024 hadi sasa, wakiwemo 481 waliokidhi vigezo kupitia Programu ya Mama Samia inayolenga kuwafikia mafundi wanagenzi 80,000 ifikapo mwaka 2027.






