Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewakutanisha Wenyeviti 45 wa Kamati za Kitaalamu za Uandaaji wa Viwango kutoka sekta mbalimbali nchini na kuwapatia mafunzo elekezi yanayolenga kuimarisha ujuzi na ufanisi wao katika uandaaji wa viwango vya kitaifa vinavyozingatia miongozo ya kimataifa.

Mafunzo hayo yamefanyika Novemba 27, 2026, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani mwaka 2026, yenye lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha mchango wa wadau katika maendeleo ya miundombinu ya ubora nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura A. Katunzi, amesema wenyeviti wa kamati hizo wana nafasi muhimu katika kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa vinakidhi mahitaji ya wadau, vinalinda afya na usalama wa watumiaji, vinatunza mazingira na kuwezesha biashara ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema kamati za kitaalamu ndizo msingi wa uandaaji wa viwango vya kitaifa, hivyo ni muhimu kwa viongozi wake kuwa na weledi, uwazi na uwezo wa kuwashirikisha wadau wenye maslahi mbalimbali katika mchakato mzima wa uandaaji wa viwango.

Dkt. Katunzi amewasisitiza wenyeviti hao kuhakikisha wanabaini mahitaji mapya ya viwango katika sekta wanazosimamia, kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia, mahitaji ya soko na vipaumbele vya taifa.

Aidha, amewataka kuweka msisitizo katika uandaaji wa viwango vinavyosaidia ukuaji wa sekta za kimkakati zikiwemo nishati jadidifu, teknolojia safi, ufanisi wa nishati, viwanda, kilimo, madini na huduma, ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesema ni muhimu pia kamati hizo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mipango na muda uliowekwa, kuongeza ushiriki wa wazalishaji, watumiaji, watafiti, taasisi za Serikali na sekta binafsi, pamoja na kufanya mapitio ya mara kwa mara ya viwango vilivyopo ili viendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Akizungumzia umuhimu wa maadhimisho ya mwaka huu, Dkt. Katunzi amesema yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Maono ya Pamoja kwa Dunia Bora: Nishati Nafuu na Safi kwa Wote,” inayosisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, endelevu na safi kwa kila mtu.

Ameeleza kuwa viwango vina mchango mkubwa katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa mifumo na teknolojia za nishati, akibainisha kuwa upatikanaji wa nishati safi na nafuu ni muhimu katika kukuza viwanda, biashara, kilimo, teknolojia na huduma za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa za shirika hilo, TBS ina wataalamu zaidi ya 500 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaoshiriki katika shughuli za uandaaji wa viwango, hali inayoonesha umuhimu wa ushirikiano wa kitaalamu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwango vinavyoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Katika maadhimisho hayo, TBS pia imepanga kutoa tuzo kwa washindi takribani 11 wa Tuzo za Ubora za mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango na juhudi za wadau katika kuimarisha ubora.

Vilevile, wenyeviti 14 wa Kamati za Kitaalamu waliotumikia nafasi hizo kwa kipindi cha miaka 15 na kuendelea wanatarajiwa kutambuliwa kwa mchango wao katika kuendeleza shughuli za uandaaji wa viwango nchini.

Mbali na mafunzo hayo, maadhimisho hayo yanajumuisha utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, maonesho na kampeni za uelimishaji katika maeneo mbalimbali ya kimkakati jijini Dar es Salaam, pamoja na mjadala wa wadau kuhusu nishati nafuu na safi kwa wote.

Dkt. Katunzi amesema mafanikio ya kamati hizo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya vikao vinavyofanyika au viwango vinavyoandaliwa pekee, bali yanapaswa kuangaliwa kupitia ubora wa viwango hivyo na mchango wake katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Amesisitiza kuwa viwango si nyaraka za kawaida, bali ni nyenzo muhimu za kimkakati katika kujenga uchumi shindani, kuvutia uwekezaji, kukuza ubunifu, kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani mwaka 2026 yanaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Ubora Duniani isemayo “Ubora Ndiyo Nguvu Inayochochea Upatikanaji na Utendaji Bora wa Nishati,” yakilenga kuonesha nafasi ya ubora katika kufanikisha upatikanaji na matumizi bora ya nishati.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa kwa hafla ya Dinner Gala itakayohudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kwa ujumla, juhudi hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na shirikishi, huku viwango bora vikitarajiwa kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu za kukuza uzalishaji, biashara na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.