NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Ulinzi wa haki na utu wa mtoto shuleni umeibuka kuwa ajenda muhimu kwa asasi za kiraia nchini, zinazotaka walimu wa shule za msingi na sekondari kupewa elimu kuhusu matumizi ya adhabu mbadala badala ya viboko, ili kujenga mazingira salama ya kujifunzia na kumwezesha kila mtoto kupata elimu bila kudhalilishwa.
Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) umesema utaimarisha elimu kwa walimu kuhusu mbinu za kurekebisha tabia za wanafunzi, pamoja na kushughulikia watoto wanaokinzana na sheria kwa kuzingatia haki zao, ikiwemo kuwawakilisha mahakamani na kuwezesha urejeshwaji wao shuleni ili waendelee na masomo.
Maazimio hayo yamejadiliwa katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 26 – 27, 2026 kikilenga kutathmini utendaji wao kwa mwaka 2026, katika kuimarisha ulinzi wa mtoto na kuhakikisha anapata elimu katika mazingira salama.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Miradi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura amezitaka asasi hizo kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuleta matokeo chanya katika jamii.
Washiriki walijadili mifumo ya kitaifa katika sekta ya elimu na namna ya kushirikiana na Serikali kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili watoto katika mazingira ya shule.
Akizungumza katika kikao hicho, Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hamisi Mayombo, amesema Wizara ya Elimu inapaswa kutoa mwongozo wa wazi kwa walimu kuhusu matumizi ya adhabu zinazozingatia haki na utu wa mtoto badala ya kutegemea viboko.
Amesema jamii inapaswa kubadili mtazamo uliojengeka kwa muda mrefu kuhusu adhabu ya viboko, akieleza kuwa mazoea ya kutumia njia hiyo hayapaswi kuwa sababu ya kuendelea nayo, hasa pale ambapo kuna mbinu nyingine zinazoweza kumsaidia mwanafunzi kurekebisha tabia.
Mwanasheria wa WILDAF, Joachim Urio, amewataka walimu kujenga mawasiliano mazuri na wanafunzi kabla ya kuchukua hatua za kinidhamu, huku akitaja kunyimwa baadhi ya fursa au vitu kwa muda unaofaa kuwa miongoni mwa njia zinazoweza kutumika kama adhabu mbadala.
Naye Meneja wa Ufuatiliaji, Tathmini, Uwajibikaji na Ujifunzaji wa HakiElimu
Irene Kanyonkole, ameitaka Wizara ya Elimu kutoa mwongozo wa utekelezaji badala ya kukaa kimya, hususan baada ya Mahakama kutoa uamuzi kuhusu kufuta adhabu viboko shuleni.
Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni kuhakikisha wanafunzi wenye changamoto za kitabia, kihisia na kijamii wanapata msaada unaostahili, kwa kuweka mikakati ya kuwasaidia kubadili mwenendo wao kwa kushirikisha walimu, wazazi na walezi.
Maazimio mengine ni kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu madhara ya makosa yao, kuwahamasisha kuomba msamaha na kurekebisha madhara waliyosababisha pale inapofaa, pamoja na kushiriki katika shughuli salama na zenye manufaa kwa shule bila udhalilishaji au kulazimishwa kufanya kazi.
Aidha, wazazi na walezi wanapaswa kushirikishwa katika kutatua changamoto za kitabia za watoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuwasaidia.
Hatua hizo zinafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, katika shauri la Samwel Maduhu Mangu dhidi ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Shauri Na. 32373 la mwaka 2025, uliotolewa Novemba 3, 2026, ambao ulifuta msingi wa kisheria wa adhabu ya viboko shuleni.
Katika uamuzi huo, Mahakama ilibaini kuwa Kanuni ya 3 ya Kanuni za Elimu kuhusu Adhabu ya Viboko za mwaka 2002 (GN Na. 294 ya 2002), ikisomwa pamoja na fasili ya adhabu ya viboko chini ya Kanuni ya 2, inakiuka Ibara ya 12(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolinda utu wa binadamu, pamoja na Ibara ya 13(6)(e) inayokataza mtu kuteswa, kupewa adhabu ya kikatili au kudhalilishwa.
Kwa msingi huo, wadau wa elimu wanasisitiza kuwa shule zinapaswa kuwa sehemu ya kumjenga mtoto kitaaluma, kitabia na kijamii, badala ya kuwa mazingira yanayoweza kumvunja moyo, kumdhalilisha au kumfanya aachane na masomo.


