Na Manka Damian, JamhuriMedia, Mbeya

MTOTO wa jinsi ya kiume aliyeibiwa akiwa na akiwa na siku kumi na nne mkazi wa Mtaa wa Iyela One Kata ya Iyela Jijini Mbeya aliyeibwa na mtu asiyejulikana jioni Aprili 29,2025 muda mfupi baada ya mama yake Neema Mkunywa alipotoka kumsindikiza mgeni amepatikana akiwa hai upenuni mwa nyumba yao Mei 15,2025 majira ya saa mbili na nusu usiku.

Neema aliyejifungua mtoto huyo wa pekee kwa njia ya upasuaji amesema alifikiwa na mgeni ambaye ni dada yake baada ya maongezi alitoka kumsindikiza umbali wa mita mia tatu lakini aliporejea hakumkuta mtoto ambaye alikuwa amemlaza sebuleni.

Baada ya kumkosa alimuuliza Aines Lwinga Mama mwenye nyumba ambaye alisema hakumuona ndipo walitoa taarifa kwa balozi Msaidizi Neva Mgode ambaye alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa Gabriel Button ambaye naye alitoa taarifa Polisi.

Kwa upande wake Gabriel Button amesema tukio hili limemsikitisha na ni la kwanza kutokea mtaani kwake huku akiwataka wazazi kuwa makini na familia zao pia kutowaami wageni wanaowatembelea.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo wananchi wameshiriki kumtafuta mtoto huyo mchanga bila mafanikio wito ukitolewa kwa yeyote anayemshuku mtu aliye na mtoto asiye wa kwake atoe taarifa Polisi au Ofisi yoyote ya Mtendaji Kata.

Baada ya kutafutwa kwa wiki tatu bila mafanikio imedaiwa mtoto huyo alitelekezwa na mwanamke ambaye hakufahamika jina wala makazi kisha kutumia mbio.

Baba Mzazi Ambele Mwampagama alijaribu kumkimbiza Mwanamke aliyetekeleza mtoto lakini hakufanikiwa ndipo taarifa ilitolewa Polisi ambao walifika kisha kumpeleka mtoto Hospitali ya Rufaa ya wazazi Meta baada ya uchunguzi mtoto amekabidhiwa kwa Mama yake.

Wazazi na familia kwa ujumla wamewashukuru Watanzania kwa maombi yao hata kufanikiwa upatikanaji mtoto akiwa hai.

Matukio ya wizi wa watoto Mkoani Mbeya yamekuwa yakijirudia rudia baadhi ya wahalifu wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.