Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MCHEZAJI wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya ameibuka tena mshindi katika mashindano ya Lina PG Tour msimu wa tatu ambayo yamefanyika kwa lengo la kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Gofu marehemu Lina Nkya.
Nkya ameibuka mshindi wa kwanza katika wachezaji wa gofu wa kulipwa huku Abdallah Yusufu akishika nafasi ya pili kwa upande huo wa wachezaji wa kulipwa na Jay Nathwani kutoka klabu ya Arusha Gymkhana akishika nafasi ya kwanza kwa upande wa wachezaji wa gofu chipukizi.
Mashindano hayo ambayo yamemalizika jana katika viwanja vya TPC Moshi mkoani Kilimanjaro yamewaleta pamoja wachezaji zaidi ya 130 kutoka klabu mbalimbali za gofu hapa nchini.

Akizungumza jana mjini Moshi mara baada ya kuibuka mshindi, Nkya alisema amekuwa mshindi wa mashindano hayo mara ya tatu mfululizo na kwamba siri kubwa ya kufanyakwake vizuri ni kujikita katika mazoezi bila kuchoka wala kukata tamaa.
Alisema Lina PG Tour imekuwa ikiwaandaa kucheza mashindano mbalimbali ya kimataifa nje ya nchi pia ni sehemu kubwa inayowaleta pamoja wachezaji wa gofu wa kulipwa, chikukizi na wale wanaocheza kwa kujifurahisha.
“Tangu mashindano ya Lina PG Tour yaanze hii ni mara ya sita nashiriki na sijawahi kukosa shindano hata moja, mashindano haya kwa sasa Tanzania ni makubwa sana yamekuwa yakutusaidia kujiandaa vizuri na mashindano mengine ya ndani na nje ya nchi.” alisema Nkya.

Hata hivyo Nkya aliwataka watanzania kuondokana na dhana ya kwamba mchezo huo wa gofu ni kwa ajili ya watu matajiri na kusisitiza kuwa mtu yeyote mwenye nia anaweza kujifunza kucheza mchezo huo na baadae kuwa mchezaji bora na tegemeo kwa taifa.
“Mimi binafsi ni mwalimu nimekuwa nikiwafundisha wachezaji chipukizi namna ya kucheza mchezo huu, wapo watu tunaowafundisha bure lengo ni kuwaingiza katika ‘game’ hii, niendelee kuwashauri watu waje waanze kujifunza gofu ili tupate wachezaji wengi wanaokwenda kuliwakilisha Taifa,” alisema Nkya
Naye Nathwani aliwataka watanzania wakiwemo vijana wanaopenda kuwa wachezaji wa gofu wazuri na wa kulipwa kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha wa kufanya mazoezi.
Alisema katika gofu hakuna miujiza bali kama mtu anataka kuwa mchezaji bora na wakilipwa basi hana budi kuhakikisha anafanya mazoezi kwa bidii bila kukata tamaa.

“Mchezo wa gofu si mwepesi ni mgumu hata mashindano haya ya Lina PG Tour ni magumu pia, lakini kama umejipanga vizuri kwa kufanya mazoezi unaweza kuibuka mshindi, hata hivyo ni wazi kuwa kama unataka kuwa mchezaji wa kulipwa ni muhimu kufanya mazoezi sana,” alisema Nathwani
Aidha Nathwani aliipongeza familia ya Said Nkya kwa kuandaa mashindano ya Lina PG Tour msimu wa tatu ambayo yamewaleta wachezaji wengi kushindana na kukuza uwezo wao.
“Nayapenda sana mashindano haya ya Lina kwa sababu yanatukutanisha na wachezaji wengi, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri katika michuano hii na mingine,” alisema
Naye mchezaji wa gofu wa kujifurahisha kutoka klabu ya gofu Lugalo jijini Dar es Salaam, Meja Chediel Msechu alisema anawapongeza waandaaji wa mashindano ambayo ambayo yamekuwa yakitoa changamoto kwa wachezaji wakubwa hasa wale wa kulipwa kuweza kushindana ili kupata nafasi ya kwenda kushiriki michuano ya kimataifa.
“Nawapongeza washindi wote katika mashindano haya, niwaombe waanadaaji waendelree kuandaa haya mashindano kwaajili ya kukuza vipaji vya mchezo wa gofu hapa nchini, niwaombe wasivunjike moyo,” alisema
Akizungumza wakati wa kufunga michuano hiyo kiongozi na miongoni mwa waandaaji wa mashindani hayo, Said Nkya (mume wa Lina), aliwashukuru wachezaji wote waliojitokeza katika mashindano hayo na kuwapongeza ambao hawakufanikiwa kushinda akiwahimiza wajitokeze mashindano mengine.
“Tunaishukuru pia klabu ya TPC hapa Moshi kwa kuturuhusu kufanyia mashindano haya katika viwanja vyao, nawashukuru timu nzima iliyoendesha mashindano haya ikiongozwa na binti yangu Yasmin Chali hakika tumefanikiwa,” alisema Said.