Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochangia kuongezeka kwa kina cha bahari na kuathiri fukwe mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Naibu wa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini Mhe. Ally Kassinge aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kujenga ukuta eneo la Pwani ya Mji wa Kilwa Kivinje ili kuzuia maji ya Bahari yanayoathiri wananchi.
Mhe. Khamis ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa fukwe zote katika ukanda wa pwani, kuendelea kutenga na kutafuta fedha kupitia Mifuko ya Usimamizi wa Mazingira na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo, Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund), GEF na GCF na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.
Kwa muktadha huo Naibu Waziri Khamis alisisitiza kuwa shughuli za ujenzi wa ukuta katika eneo hilo la pwani zitaanza kutekelezwa baada ya fedha kupatikana.
Halikadhalika, alihimiza uongozi na wananchi wa Kilwa Kivinje kuendelea kuongeza jitihada za kutunza mazingira ya maeneo ya ufukwe kwa kudhibiti shughuli zisizoendelevu za kibinadamu kwa kuongeza jitihada za kuhifadhi mazingira na upandaji wa miti kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Katika hatua nyingine Mhe. Khamis alisema mradi wa ujenzi wa ukuta na matuta unaotekelezwa kwenye maeneo ya fukwe za bahari ya hindi eneo la Sipwese Mkoa wa Kusini Pemba umefikia asilimia 99.
Alibainisha hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Asya Mwadini Mohammed aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa mradi huo utakamilika lini ili kuwanusuru wananchi kwa changamoto ya kuingiliwa na maji ya bahari.
Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis kutokana na kufikia hatua hiyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kukabidhi mradi huo kwa wananchi hivi karibuni.
Pia, Naibu Waziri aliwasihi wananchi kuendelea kupanda miti hasa aina ya mikoko na kuacha kuacha kukata miti pamoja na kufanya shughuli zinazoharibu mazingira.

Alitoa rai hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalimu aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira hasa kwenye maeneo ya bahari yanayotumika katika shughuli za uchumi wa buluu.
“Uchumi wa buluu ni pamoja na shughuli mbalimbali ndani ya bahari zikiwemo uvuvi, ulimaji wa mwani na masuala ya utafiti wa kwa ajili ya ugunduzi wa mafuta na gesi, kwahiyo shughuli hizi zimekuwa zikiharibu mazingira kwa namna ama nyingine kwa kiasi fulani, mheshimiwa tumechukua hatua mbalimbali zikiwemo kutoa elimu kwa wananchi,” alisisitiza.
