Na Lookman Miraji, JamhuriMedia,

Siku ya Katiba ya Denmark ama pia maarufu kwa jina la (GRUNDLOVSDAG ) ni siku muhimu inayohusiana na historia ya katiba ya nchi hiyo. Siku hii inahusiana na kupitishwa kwa katiba ya kwanza ya Denmark mwaka 1849, ambayo ilianzisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia na kumaliza utawala wa kifalme wa kiabsoluti.

Siku hiyo ambayo huadhimishwa kila ifikapo Juni 5 kila mwaka inabaki kuwa tarehe muhimu katika jamii ya Denmark ikiashiria msingi wa demokrasia na haki za kiraia nchini humo.

Inapoelezewa historia ya katiba ya Denmark inaturejesha katika mwaka 1849, wakati katiba ya kwanza ya kidemokrasia ilipopitishwa. Kabla ya hapo, Denmark ilikuwa chini ya utawala wa kifalme wa kiabsoluti. Katiba ya 1849 ilianzisha mfumo wa utawala wa kikatiba, ikitoa haki za kiraia na kuanzisha bunge la kidemokrasia.

Baadaye, katiba hii ilifanyiwa marekebisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na mabadiliko makubwa mwaka 1953, ambapo mfumo wa kifalme wa Denmark ulirekebishwa na kuruhusu wanawake kurithi kiti cha ufalme. Pia, mabadiliko hayo yalifuta Baraza la Taifa la Denmark na kuimarisha mamlaka ya Bunge la Denmark (Folketinget).

Katiba ya Denmark imeendelea kuwa msingi wa demokrasia ya nchi hiyo, ikihakikisha uhuru wa wananchi na utawala wa sheria. Ikiwa na historia ndefu ya mageuzi, katiba hii imekuwa mfano wa utawala wa kidemokrasia katika Ulaya.

Katiba ya Denmark, iliyopitishwa rasmi mwaka 1849, katiba iliyoanzisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia na kuhakikisha uhuru wa wananchi katika masuala ya kisiasa na kijamii.

Siku hii pia hutumiwa kama fursa ya kutafakari maendeleo ya demokrasia na kuhamasisha wananchi kuhusu haki zao za kikatiba. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Taasisi ya Vyama na Demokrasia Denmark, demokrasia nchini Denmark imejengwa juu ya misingi ya uhuru wa kisiasa na ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya kitaifa. Hii inaonyesha jinsi katiba inavyohakikisha uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika utawala.

Siku ya Katiba ni tukio la kitaifa linaloadhimishwa kwa sherehe na mijadala kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii, likiwa na lengo la kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu demokrasia na utawala bora. Hii hasaidia kuendeleza utamaduni wa kisiasa unaozingatia haki na usawa katika jamii.

Kupitia ubalozi wa Denmark uliopo hapa nchini umeadhimisha siku hiyo, ukiwaleta pamoja washirika wake wengine , wawakilishi wa mashirika ya kimataifa pamoja na baadhi ya waandamizi wa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Katika hafla hiyo iliyoongozwa na balozi wa Denmark hapa nchini, Jesper Kammersgaard ilihudhuriwa na Waziri wa mambo ya nnje na ushrikiano wa Afrika Mashariki , Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyehudhuria akiwa kama mgeni rasmi wa shughuli hizo.

Katika hotuba yake Waziri Kombo ameelezea sehemu ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Denmark kwani yameendelea kuwa imara kwa zaidi ya miongo sita mpaka sasa.

Akiyaelezea mahusiano hayo, Waziri Kombo amesema kuwa sehemu ya mahusiano hayo si tu ya kuimarisha maono bali yamepelekea kuwepo kwa maeneo halisi ya ushirikiano huku akielezea ushirikiano kati ya Tanzania na Denmark katika sekta ya afya kuongeza kuwa ushirikiano wa kiuchumi unabaki kuwa kipaumbele kikuu.

“Mahusiano haya siyo tu kuimarisha maono yetu ya pamoja bali pia yamepelekea maeneo halisi ya ushirikiano, ambayo tumekusudia kuyatekeleza kwa kuwapo kwa ushirikiano na maendeleo. Ningependa pia kutambua jukumu la kihistoria la Denmark katika kusaidia sekta ya afya ya Tanzania. Kupitia Mpango wa Usaidizi wa Sekta ya Afya (HSPS), taasisi nyingi za umma na binafsi zimefaidika kutoka hospitali za serikali hadi mashirika kama CSSC, APHFTA, CCBRT, na mengineyo. Ushirikiano wao na maafisa wetu wa afya umefungua milango mipya ya ushirikiano katika udhibiti wa dawa na maendeleo ya mifumo ya huduma za afya ambayo ni muhimu kwa ustawi wa watu wetu. “

Mbali na hayo katika sekta ya afya, Waziri Kombo ameonesha kufurahishwa na ongezeko la idadi ya watalii wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini huku akitoa wito kwa watalii wengi zaidi kutoka Denmark kutembelea vivutio nchini.

” Kuhusiana na utalii, tunafurahi kwa kuongezeka kwa hamu miongoni mwa wageni kutoka Denmark. Idadi ya watalii wanaotembelea kutoka Denmark iliongezeka kutoka 14,071 mwaka 2022 hadi 15,036 mwaka 2024, ambayo ni mwenendo mzuri wa kuongezeka. Nawaalika kwa moyo mkunjufu watalii wengi zaidi wa Denmark kuja kushuhudia vivutio vya asili na tamaduni vya kuvutia vya Tanzania kuanzia Kilimanjaro na Serengeti hadi visiwa vyenye uchawi vya Zanzibar.”

Aidha, Waziri Kombo pia amesema kuwa serikali inaendelea kujitolea kuwezesha na kulinda uwekezaji na kuhakikisha kwamba ni wa manufaa kwa pande zote.

” Tanzania inatoa uchumi thabiti unaokua na mazingira ya biashara ya wazi. Serikali yetu inaendelea kujitolea kuwezesha na kulinda uwekezaji, kuhakikisha kwamba ni wa manufaa kwa pande zote na endelevu kwa muda mrefu.” Alisema.

Kwa upande wake nae Balozi wa Denmark nchini ,Jesper Kammersgaard ameonesha kufurahishwa na mwenendo wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Denmark na Tanzania ambapo pia ameahidi kuendelea kudumisha uhusiano huo na kuwa wenye tija kwa pande zote mbili.

Maadhimisho ya siku ya katiba ya Denmark yalifanyika ijumaa ya Juni 05 katika makazi rasmi ya Balozi wa Denmark yalioko jijini Dar es salaam.