Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetunukiwa tuzo maalum ya ushirikishaji jamii katika ujenzi wa barabara yaani ” People Centered Design Approach”.

Ushirikishaji huo ni kuhakikisha usanifu unajumuisha mawazo, mapendekezo na mahitaji maalum kwa ajili ya jamii itakayohudumiwa na barabara husika baada ya kujengwa hususani maeneo ya shughuli za kijamii kama shule, masoko na huduma za afya (hospitali, vituo vya afya, zahanati na kliniki).

Tuzo hiyo maalum imetolewa na Taasisi ya Kimataifa ya ‘FIA Foundation’ kwa kushirikiana na AMEND katika kongamano la Kikanda la Afrika lililofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam lililohudhuriwa na nchi mbalimbali ikiwemo Ghana, Ivory Coast, Kenya, Zambia, Msumbiji, Afrika ya Kusini, Sao Tome, Madagascar na mwenyeji Tanzania.

TARURA imeshiriki kongamano hilo kwa kutoa elimu kwa nchi mbalimbali za kiafrika ili kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakuwa salama kwa watumiaji hususani watoto wa shule.