Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kampuni tanzu ya Huaxin Group, Maweni Limestone (MLL-Tanzania), imepiga hatua kubwa kibiashara kwa kuzindua bidhaa mpya ya saruji ijulikanayo kama ‘Newta’ inayotarajiwa kuboresha sekta ya ujenzi nchini.⁸

Haya yanajiri wakati miradi mingi ya ujenzi ikiendelea kutekelezwa inayohitaji bidhaa bora kama za Newta katika kuitekeleza.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa kampuni ya Huaxin Group, Wang Jiajun, amesema uongozi umefanya utafiti wa kina na kufikia uamuzi wa kuja na wazo la kuzalisha bidhaa hiyo mpya ambayo anasema inatarajiwa kukidhi mahitaji katika sekta ya ujenzi.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Huaxin Group ambayo ni kampuni mama ya Maweni Limestone (MLL-Tanzania, Wang Jiajun (aliyevaa koti), akiongoza watendaji wengine katika uzinduzi wa saruji mpya ijulikanayo kwa jina la Newta. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam wiki hii.

“Matokeo ya utafiti wetu umewezesha kupata bidhaa ya hali ya juu katika soko la ujenzi nchini, ambayo ni rahisi kutumia hata kwa mafundi wapya wanaoingia kazini kwa mara ya kwanza, kwa kuwa bidhaa hii mpya itawawezesha kufanya umaliziaji wa shughuli za ujenzi vizuri,” amesema.


Jiajun anasema bidhaa hiyo mpya ina uimara ambao utawawezesha makandarasi na wamiliki wa miradi itakayotekelezwa kuokoa muda wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo kutokana na ukweli kuwa bidhaa hiyo mpya inakauka mapema na hivyo kutoa fursa ya mafundi kuendelea na shughuli zingine za umaliziaji.

Makamu huyo wa Rais wa Kampuni ya Huaxin Group alitoa rai kwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa bidhaa hiyo mpya kuhakikisha wanatumia fursa zitakazotokana na Newta ambayo alisema muonekano wake ni mzuri na ambao utaifanya nyumba kuwa ya kuvutia.


Bidhaa hiyo mpya alisema inazalishwa katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko eneo la Mkuranga mkoani Pwani, sambamba na bidhaa nyingine zinazozalishwa na kampuni hiyo kubwa na kuongeza kuwa inatarajiwa kupatikana maeneo yote hapa nchini kutokana na kampuni hiyo kuwa na miundombinu itakayowezesha kuisafirisha bidhaa hiyo nchini kote na kwa wakati.

“Tuna imani na bidhaa hii mpya na ni matumaini yetu kuwa Watanzania wataipokea vyema na kuthamini matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wa kampuni yetu,” alisema.

Bw. Jiajun aliishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo kuvutia wafanyabiashara wengi kuja kuwekeza Tanzania.

“Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha jumuiya ya wafanyabiashara inakuwa na mazingira mazuri ya kuwekeza; hili linadhihirishwa na uamuzi wa kampuni yetu ambayo ni moja ya wazalishaji wakubwa wa saruji duniani kuja kuwekeza hapa nchini”, alisema na kuongeza, tuna kiwanda cha MLL-Tanga kilichoko mkoani Tanga na kile cha Mkuranga kilichoko mkoani Pwani.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Maweni Limestone Ltd, Louis Liu, Mkuu wa kitengo cha Biashara wa kampuni ya Huaxin Group kwa ngazi ya kimataifa, Jessica Ma, mawakala mbalimbali wa kibiashara, viongozi wa serikali na wadau wengine wa sekta ya ujenzi hapa nchini.

Huaxin Cement MLL-Tanzania, ilianza kuwekeza nchini Tanzania mwaka wa 2019, na ni kampuni tanzu ya kampuni ya Huaxin Group iliyoanzishwa mwaka wa 1907 na ambayo ni wazalishaji wakuu wa vifaa vya ujenzi kutoka China. Huaxin Group inafanya kazi katika nchi zaidi ya 18 kupitia kampuni zake tanzu zaidi ya 300.