Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2025, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesisitiza dhamira yake ya kutoa huduma bora, zenye kuzingatia weledi, uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya teknolojia kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo jijini Dodoma June 16,2025  Mkurugenzi mkuu wa Ewura Dkt.James Andilile amesema EWURA itaendelea kujielekeza katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kwa kuhakikisha kuwa huduma zote za nishati na maji zinafikia walengwa kwa ubora unaostahili.

“Huduma kwa wananchi siyo fadhila, ni haki yao ya msingi,kama Taasisi ya Serikali, tunatambua wajibu wetu kwa Watanzania na ndiyo maana tunaendelea kujipanga kutoa huduma bora kwa kutumia mifumo ya kidijitali na kuimarisha usimamizi katika sekta tunazozihudumia,” amesema  .

Ameongeza kuwa katika kipindi  cha wiki ya utumishi wa umma, EWURA imekuwa ikikutana moja kwa moja na wananchi ili kusikiliza changamoto, kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wao, na kueleza namna taasisi hiyo inavyosimamia bei, ubora, na upatikanaji wa huduma za mafuta, umeme, gesi asilia, na maji safi na usafi wa mazingira.

Aidha, amesema EWURA inatambua kwamba huduma bora kwa umma ni chachu ya ustawi wa jamii na uchumi wa nchi, hivyo itaendelea kusimamia misingi ya utawala bora ikiwemo uwazi, uwajibikaji na kushirikisha wananchi katika maamuzi.

Katika hatua nyingine,Dkt.Andilile ametoa wito kwa jamii  kuhakikisha wanatumia wiki ya utumishi kama jukwaa la kupata taarifa mbalimbali za Ewura na kueleza kuwa hali hiyo itaboresha mifumo ya utoaji huduma na kujifunza kutoka kwa wadau na wananchi.

Pamoja mambo mengine kiongozi huyo amesisitiza kuwa EWURA iko tayari kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara wa vituo vya mafuta ya Taa, petroli au dizeli watakao fanya bishara kea kuchakachuo bidhaa hizo. 

Pia wafanya bishara hao wametakiwa kuzingatia bei elekezi kwa kumuuzia mafuta mteja kadri ya mahitaji yake na si vinginevyo. 

Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha uwajibikaji, maadili ya kazi, pamoja na kutoa nafasi kwa taasisi za umma kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma.