Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahamasisha wasanii na Watanzania kwa ujumla kujisajili kwenye mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST) ili kunufaika na zabuni za asilimia 30 zilizotengwa kwa makundi maalum.

Wito huo umetolewa Julai 5, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba alipokuwa akizungumza na waigizaji wa tamthilia ya Kombolela, walipotembelea kwenye Banda lao lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata uelewa kuhusu mfumo wa NeST.

Alisema tayari zabuni zenye thamani ya Shilingi Bilioni 16 zimeshatolewa kwa makundi maalum, huku lengo kuu likiwa ni kufikia thamani ya Shilingi Trilioni 5.

“Tumesema taasisi zote za ununuzi zitenge asilimia 30 kwa makundi maalum. Na huu ni wakati sahihi zaidi kwa Watanzania kujitokeza kwani mwaka mpya wa fedha umeanza, na tenda nyingi zimetangazwa tayari kupitia NeST,” alisema Simba.

Alieleza kuwa mfumo wa NeST unapatikana kwa urahisi kupitia intaneti na kila Mtanzania mwenye sifa anaweza kufuatilia tenda zote za Serikali moja kwa moja.

“Miaka 20 iliyopita watu hawakujua tenda za Serikali zinapatikana vipi. Leo ukiwa na bando lako tu, unafungua NeST, unaona kila tenda ya Serikali iliyotangazwa,” alisema.

Amehimiza vikundi vya sanaa na wajasiriamali kujisajili kwa kuandaa Katiba ya kikundi, leseni halali, na nyaraka muhimu nyingine.

Aidha, amesema kwa wale wasioweza kufika Sabasaba, PPRA imefungua ofisi za kanda sita kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa karibu.

Simba amesema NeST ni suluhisho la uwazi, ushindani na fursa halali kwa Watanzania wote, hivyo hakuna sababu ya kukosa zabuni kama vigezo vimekidhi.