Adaiwa kuiba misalaba makaburini

KATAVI

Na Walter Mguluchuma

Polisi mkoani Katavi wanamshikilia mkazi wa Majengo mjini Mpanda, Mashaka Sokoni (28), kwa tuhuma za kukutwa na vipande 35 vya vyuma vya misalaba ya makaburi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga, amesema Sokoni amekamatwa usiku wa Agosti 7, mwaka huu wakati akiuza vipande hivyo kama chuma chakavu.

“Sokoni alikamatwa na kikosi kazi maalumu cha Jeshi la Polisi kilichokuwa kikifanya doria. Walimtilia shaka baada ya kumuona usiku ule akiwa amebea kifurushi.

“Baada ya kufanyiwa upekuzi wakabaini kuwa ndani ya mfuko huo kuna vipande 35 vya vyuma vya misalaba, majina ya marehemu yakiwa yameshafutwa,” anasema Kuzaga.

Kamanda Kuzaga anasema baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kuiba vyuma vya misalaba ya makaburi ya Nsemulwa, nje kidogo ya mji wa Mpanda, akidai ni kwa lengo la kujipatia kipato.

Amesema polisi watafanya msako mkali kuwakamata wote wenye tabia ya kujipatia kipato isivyo halali kwa kufanya vitendo vya aibu katika jamii.

Mtuhumiwa bado anashikiliwa kwa mahojiano zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.