Na Joe Beda Rupia

Keki. Inadhaniwa kuwa ni moja kati ya vyakula vitamu duniani. Wakati mwingine hutumika kama alama ya upendo na umoja.

Keki. Shughuli bila keki haijakamilika. Harusi au sherehe za kuzaliwa bila keki! Hiyo haiwezi kuwa shughuli. Haijakamilika.

Keki si chakula cha kushibisha. Unakula kwa hamu tu ili kujumuika na wengine wanaoshiriki katika shughuli husika.

Kula keki hiyo ni muhimu. Kunaonyesha mshikamano. Hata sisi tusiopenda vitu vitamu, hulazimika kuonja japo kakipande kadooogo ka keki.

Keki si chakula cha kawaida sana. Huliwa kwa nyakati fulani tu hata kama wapo wanaokula mara kwa mara, au kila siku.

Simulizi ya mapinduzi ya Ufaransa inachagizwa na kauli inayodaiwa kutolewa kipindi fulani mwaka 1789 na Marie-Antoinette, mke wa Mfalme wa Ufaransa, Louis XVI, kuhusu keki.

Historia inadai kwamba wakati waandamanaji wakipiga kelele barabarani hadi karibu na jumba la mfalme wakilalamikia kukosa ‘mkate’ (chakula), Marie-Antoinette akashangaa na kuwauliza walinzi wake akisema: “Kama hawana mkate, kwa nini wasile keki?”

Jamani. Mkate wenyewe shida, keki itapatikana vipi? Inadaiwa kuwa walinzi wake mwenyewe walikasirika na kuruhusu waandamanaji kumshambulia, hatimaye kumuua na kufanikisha mapinduzi yale ya kihistoria.

Keki hiyo. Lakini pia ‘keki’ ni dhana. ‘Keki ya taifa’ si keki ya ngano! Keki ya taifa si chakula cha kuweka mdomoni na kusikia utamu wake! Ni dhana.

Aliposhinda urais mwaka 1995, wakati akijiandaa kuunda Baraza la Mawaziri, Rais wa Tatu wa Tanzania, Ben Mkapa, alidhani ni busara kwenda Msasani (Butiama?) kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuomba ushauri nani na nani wawemo kwenye baraza hilo.

Katika kitabu chake, Mkapa anamnukuu Mwalimu akimweleza: “… it is your Government and it is your cabinet. Go and form it.”

Pamoja na maneno au maelekezo hayo, Mwalimu akamwambia Mkapa kuwa kuna mambo mawili ya kutazama kwa umakini katika kuunda Baraza la Mawaziri.

Kwamba, taifa hili kuna dini na pia kuna makabila. Kwamba katika kutengeneza serikali, hayo mawili lazima yatazamwe kwa umakini. Kuwe na uwiano fulani katika hayo ndani ya serikali.

Nadhani Mkapa alielewa. Akaunda serikali yake na kutawala kwa miaka yake aliyopangiwa na Mungu na kumaliza. Mungu amrehemu.

Kama Mkapa alifanikiwa kugawa ‘madaraka’ kwa namna alivyoelekezwa au kuaswa na Mwalimu, basi huenda ilikuwa ni kutokana na ukweli kwamba miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2000, kulikuwa na mikoa ‘asilia’.

Baadaye mikoa ikaanza kugawanywa kwa matakwa ya kisiasa. Majimbo yanagawanywa ili kina fulani wapate ubunge. Wilaya zinagawanywa na kuongezeka ili wengine wapate ukuu wa wilaya na ukurugenzi. Mikoa nayo vivyo hivyo.

Migao hiyo mipya imevuruga uasili uliokuwa umeanza kujengeka. Imeweka mipaka mipya ya kiutawala. Imemega makabila. Mimi hata sielewi!

Uandishi wa habari wakati mwingine huwa mgumu sana. Hivi Tanzania kuna makabila mangapi? Wanasema ni 128. Wengine wanasema ni zaidi ya 120. Hakuna namba kamili. Lakini tunachokubaliana sote ni kwamba, yapo mengi.

Ugumu wa kazi hii nilikumbana nao Juni mwaka huu nikiwa Kwa Moromboo, Arusha. Huko nikakutana na rafiki yangu mmoja wa siku nyingi sana.

Akaanzisha hoja ya ‘keki ya taifa’. Mwenyewe anasema kabila lao limetengwa na hawana uwakilishi kabisa serikalini. Wamesahaulika kwenye ‘hafla’ ya keki ya taifa wanayoshiriki kuitengeneza.

Moyoni nikashituka. Nikawaza: “Wewe ‘Mnyakyusa’ (ndivyo alivyokuwa akijiita na tulivyokuwa tukimwita mtaani kwetu miaka ileee!) unasema mmetengwa?”

Kama anasoma mawazo yangu vile! Akasema: “Hebu niambie. Kuna Mburushi gani serikalini? Yaani ni kama hatuna mchango kwa taifa letu. Sisi kabila letu limesahaulika kabisa kabisa, yaani utadhani si Watanzania!”

Hapo sikuweza kuvumilia, nikamuuliza: “Kwani Waburushi nao ni kabila?” Akanishangaa na kunieleza (kwa mara ya kwanza maishani mwangu) kuwa Waburushi ni miongoni mwa makabila 128 ya Tanzania!

Aise! Kama ni hivyo basi kweli wamesahaulika hata kwenye medulla oblongata yangu hawamo. Sikuongeza neno. Kinywaji kikaendelea na stori kibao kwa kuwa hatukuwa tumeonana siku nyingi na siku hiyo tulikuwa nje ya Dar es Salaam. Hatuna majukumu mengi.

Baada ya muda fulani, tukiwa tayari tumeshapata nyama ya kondoo kwa Moromboo, nikarejesha tena hoja ya mgawanyo wa keki ya taifa na kutengwa kwa makabila madogo nchini kama Waburushi.

Jamaa yangu akasema: “Nyerere hakuyaacha makabila hata madogo madogo. Unajua hata Wahindi walikuwamo kwenye serikali yake!”

Baada ya kucheka, nikadhani sasa muda wa kuondoka eneo hilo umewadia. Yaani huyu rafiki yangu anataka sasa na Wahindi kuwaingiza kwenye makabila 128 ya Tanzania?

Nikatazama chupa yake; kumbe naye anakunywa Safari kama mimi! Sasa vipi? Mbona imemkolea kuliko kawaida?

“Sikiliza Joze, Wahindi ni miongoni mwa jamii ndogo hapa nchini. Achana na hawa wanaokuja, wapo waliozaliwa Tanzania. Wamesoma hapa na hapa ndipo kwao hata Kenya hawajawahi kufika.

“Hii jamii kwa nini inatengwa na nyie (waandishi wa habari) mpo kimya tu? Unadhani hawana nafasi ya kutoa mchango kwa taifa? Nyerere alilifahamu hilo ndiyo maana alikuwa na akina Amir Jamal bro!

Nikaona ni vema nikaongeza walau ‘moja moja’, maana sasa ninaanza kumuelewa, hata kukubaliana naye. Nikaanza kuona point kwa mbaaaali!

Naam! Kuna jamii zimetengwa. Kuna watu wamesahaulika kwenye kugawana keki ya taifa. Keki ya taifa hii keki ya dhana.

Nikaanza kuwaza, hivi mgawanyo wa Baraza la Mawaziri kwa sasa ukoje? Hilo nikaliweka pembeni ili mazungumzo yaendelee mezani kwetu kwa Moromboo.

Siku chache baadaye, nikaanza kutazama mgawanyo wa baraza la sasa. Kwa kanda. Kwa mkoa. Nikakuta kumbe wakati ninamshangaa rafiki yangu ‘Mburushi’ aliyedai kutengwa, kumbe na mimi nimetengwa sina habari!

Rukwa. Katavi. Naibu Waziri mmoja tu! Ushauri wa Baba wa Taifa umeishia kwa Mkapa tu aise! Wakuu wa mikoa je? Wa wilaya? Ma-DED? Nikaona kuendelea kuwaza hivi ni kuendekeza ukabila karne ya 21 wakati hata kutambika sijui wanafanyaje.

By Jamhuri