Watoto zaidi ya milioni moja wamo katika maandalizi ya mitihani ya kumaliza masomo ya shule ya msingi inayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao nchi nzima.

Maana yake ni kwamba ndani ya miezi mitatu tu baada ya hapo, watoto hawa watahitaji nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za umma na zile za binafsi.

Kwa kulitambua hilo, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amewakumbusha wakuu wa mikoa kuanza mara moja ujenzi wa madarasa tayari kuwapokea watoto hao.

Ummy alitumia nafasi aliyopewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akizungumza na viongozi hao kwa njia ya video kutoka Dodoma, kuwakumbusha wajibu wao huo.

Si vibaya kwa kiongozi wa juu kuwakumbusha wasaidizi wake wajibu wao hasa kama miongoni mwao kuna wageni wamepewa nafasi hizo kwa mara ya kwanza.

Hapa ni muhimu kumpongeza Waziri Ummy kwa kuwa ingawa ni mara yake ya kwanza kushika nafasi katika wizara inayowajibika na miundombinu ya shule, na amekumbuka mapema kero hiyo.

Upungufu wa madarasa nyakati za mwanzoni mwa mwaka imekuwa ni kero ya kawaida inayojirudia mwaka hadi mwaka kana kwamba serikali haifahamu kuwa wapo watoto wanaohitaji kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza.

Hii imekuwa ni aibu na sasa Ummy hataki kuiona ikijirudia Januari 2022. Kitendo cha watoto waliofaulu kulazimika kukaa nyumbani wakisubiri ujenzi wa miundombinu ya shule kinawaumiza kisaikolojia, huku kikiwathibitishia akilini mwao uzembe wa wazi wa viongozi wa taifa letu.

Sisi tunajiuliza, ni wakuu wa mikoa wangapi waliokuwa wakikumbuka jukumu hilo wakati huu, mwezi mmoja kabla watoto hawajafanya mitihani ya kumaliza darasa la saba?

Na je, baada ya kukumbushwa, ni hatua gani wanazichukua kuhakikisha kuwa aibu hii haitokei tena mwakani? Je, wanafahamu kuwa si madarasa tu yanayohitajika bali pia vyoo, madawati, nyumba za walimu na vifaa vingine vingi?

Tungependa kusikia na kuona Waziri Ummy akipiga hatua nyingine mbele kwa kuweka wazi adhabu atakayopata kiongozi yeyote atakayeshindwa kujiandaa kuwapatia watoto hao mahitaji yao ya kielimu.

Kwa upande mwingine, iwepo zawadi au motisha kwa watakaofanya vizuri na kuwaingiza sekondari watoto wote ndani ya Januari mwakani bila kupoteza muda.

By Jamhuri