Afisa uchaguzi Kenya aliyetoweka apatikana akiwa amefariki

ALIYEKUWA msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha kupigia kura katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, amepatikana akiwa amefariki siku chache baada ya familia yake kuripoti kuwa ametoweka, vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti.

Mwili wa Daniel Mbolu Musyoka umepatikana katika msitu wa Loitoktok chini ya Mlima Kilimanjaro karibu na mpaka na Tanzania, ripoti zinamnukuu mkuu wa polisi akisema.

Mwili huo ulitambuliwa na dada zake wawili, gazeti la Daily Nation linaongeza. Inasema mwili huo ulipatikana na wafugaji na ulikuwa na alama zinazoonyesha alifanyiwa mateso.

Musyoka alikuwa afisa msimamizi katika eneo la Embakasi Mashariki jijini Nairobi.

Kutoweka kwake kuliripotiwa Ijumaa iliyopita na Tume ya Uchaguzi, ambayo ilisema alitoweka akiwa kazini katika kituo cha kujumlisha kura.