Afya ya Rais Sambi yadhoofu

#Anyimwa chanjo UVIKO-19, wananchi walalamika

# Miaka 3 na nusu amefungiwa chumbani kizuizini

#Aililia Tanzania, jumuiya ya kimataifa wamsaidie

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Afya ya aliyekuwa Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi, anayeteswa kizuizini nchini humo inazidi kuwa mbaya, JAMHURI limethibitishiwa.

Sambi yumo kizuizini kwa miaka mitatu na nusu sasa kwa amri ya Rais wa Visiwa hivyo, Kanali Azali Assoumani.

Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vya habari ndani ya Serikali ya Comoro zinasema licha ya Sambi kudhoofu, Serikali ya Rais Assoumani imeendelea na msimamo wa kumzuia hata asipate chanjo ya ugonjwa wa UVIKO-19 ambao unaendelea kuua maelfu ya watu duniani.

“Kunyimwa haki ya kupata chanjo ya UVIKO-19 kunazidi kumweka kwenye mazingira magumu zaidi kiafya. Ingawa ndugu hawaruhusiwi kumtembelea, tuna shaka na watendaji wachache wa serikali wanaomlinda akiwa kizuizini huenda wakawa chanzo cha yeye kupata maambukizi,” kimesema chanzo chetu.

Kwa miaka miwili sasa maombi ya Sambi kupatiwa matibabu nchini Tanzania yamegonga mwamba licha ya Mahakama ya Juu nchini humo kutoa kibali cha kwenda kutibiwa.

Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, aliridhia Sambi atibiwe nchini Tanzania kwa gharama za Tanzania, lakini akiwa tayari ameshapata kibali cha Mahakama na kukatiwa tiketi, Rais Assoumani alitoa amri ya kufuta ruhusa hiyo. Nakala ya tiketi ya Shirika la Ndege la Kenya iliyokuwa imeshalipiwa kwa safari ya Sambi ya matibabu, lakini ikazuiwa kwa amri ya Rais Assoumani, imeambatanishwa kwenye habari hii.

Mkurugenzi wa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Emmanuel Buhohela, amezungumza na JAMHURI kuhusu kilio cha Rais Sambi na kusema: “Hilo suala liko juu ya mamlaka yangu, naomba nipate maelekezo ya namna lilivyo na baadaye naweza kuwa kwenye nafasi ya kulizungumzia. Kwa sasa sina maelezo, maana liko kwenye mamlaka ya juu.”

Kwa miaka mitatu na nusu Sambi ametengwa na dunia. Amepigwa marufuku kuonana na mkewe, watoto na mtu yeyote awaye. Mtu pekee anayeonana naye ni mtoto wa dada yake.

“Ndugu zangu hatuonani, wengine wamefariki dunia lakini nimenyimwa haki ya kushiriki mazishi.

“Nimefungiwa kwenye selo ndogo nyumbani, nanyimwa haki zote za msingi ambazo mtuhumiwa au mfungwa kama mimi nastahili kuzipata kwa mujibu wa sheria za Comoro na kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.

“Afya yangu imedhoofu, nimenyimwa matibabu kwa muda wote huo licha ya kutakiwa kuonana na madaktari na kupewa matibabu. Hii ndiyo sababu kuu iliyonifanya mheshimiwa nikuandikie barua hii ili unisaidie niweze kutibiwa.

“Daktari wangu Said Ali Petit, baada ya kunichunguza mara kadhaa ameshauri nipate vipimo na matibabu zaidi, lakini nimezuiwa kabisa. Hata jaji anayechunguza shauri langu Januari 2, 2020 alitoa kibali nipate matibabu, lakini uamuzi wake umepuuzwa,” analalamika Sambi kwenye barua aliyowahi kumwandiki Rais Samia Suluhu Hassan.

Duru za kidiplomasia zinaeleza kuwa Sambi ameendelea kuililia jumuiya ya kimataifa imsaidie aondokane na mateso anayopata kizuizini.

Kwa mara nyingine, Novemba, mwaka huu alimwandikia barua Rais Samia, ambako pamoja na kumshukuru kwa kulishughulikia suala lake, alimuomba asife moyo, badala yake aendelee kupambana ili Rais Assoumani amrejeshee uhuru wake.

Anamshukuru Rais Samia kwa kumtuma Rais mstaafu Jakaya Kikwete kushughulikia suala hili ili haki yake ipatikane.

Kwenye barua ya pili, Sambi anasema: “Napenda kukuhakikishia kuwa kwa miaka miwili nimekuwa sipati matibabu…Rais Assoumani amekuwa akipotosha kwa kudai kwamba nimewekwa kizuizini kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Comoro. Sheria zenywe haziruhusu mtu kuwekwa kizuizini kwa miezi minane lakini mimi sasa niko kizuizini kwa miaka mitatu na nusu. Januari 2, 2020 Mahakama ilitoa uamuzi wa mimi kupatiwa matibabu, lakini mamlaka ya Comoro ikafuta uamuzi huo kwa maelekezo ya Rais Assoumani.

“Kwa hakika sina hakika kama kuna siku nitapata tena uhuru wangu kwa sababu mamlaka ya Serikali ya Comoro inasema naweza kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu kadiri inavyotaka. Shaka yangu kuu kwa hili ni kutokana na serikali kutojali wala kuheshimu sheria za Comoro wala za kimataifa,” analalamika Sambi.

Ametoa mwito kwa Rais Samia kumpelekea wanasheria ili waungane na wenzao wanaomtetea kwenye sakata hili ambalo yeye anasema ni la kisiasa.

Anathibitisha hilo kwa maelezo kwamba tangu awekwe kizuizini, madai ya serikali ni kwamba anatuhumiwa kuhusika kwenye matumizi mabaya ya rasilimali za umma, na rushwa.

“Mheshimiwa Rais, kama nilivyosema mara zote, madai dhidi yangu ni ya uongo, na ndiyo maana nimekuomba ulete wanasheria unaowaamini ili wapate ukweli juu ya kubambikiwa kwangu mashitaka ya uongo na kuniweka kizuizini kwa miaka mitatu na nusu sasa,” anasema Rais mstaafu Sambi.

Hatua ya Sambi kumuomba Rais Samia aingilie kati kumnusuru imetokana na Rais Assoumani kukaidi maombi ya Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), taasisi za kitaifa na kimataifa, na watu maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika.

Rais mstaafu Sambi pia ameiandikia AU – Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Mahamat, akiomba Umoja huo usaidie kumrejeshea uhuru aliopokwa na Rais Assoumani. 

Anasema Mei 12, 2018, alijitokeza hadharani kupinga hatua ya Rais Assoumani ya kubadili Katiba ya Comoro ili kumwezesha kuendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2029. Hatua hiyo, anasema ilikuwa inafuta utaratibu wa kikatiba wa kuwa na urais wa mzunguko kwa kila kisiwa kwa miaka mitano.

Mei 18, 2018 alikamatwa na kuwekwa kizuizini nyumbani kwake kwa amri iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

Hatua hiyo anasema ni kinyume cha sheria, kwani mwenye mamlaka hayo ni jaji. Anasema licha ya mamlaka za dola kutambua kuwa kuwekwa kwake kizuizini ni kinyume cha sheria, ziliridhia pengine kwa hofu na hila.

Sambi anasema watu mbalimbali wamezuiwa kumtembelea, akitoa mfano kuzuiwa kwa Balozi wa Marekani nchini Comoro ambaye alitaka kufanya hivyo, lakini akazuiwa.

Mwaka 2001 visiwa vitatu viliunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Comoro. Katiba hiyo, pamoja na mambo mengine, ilianzisha utaratibu wa mzunguko wa urais katika visiwa hivyo kwa miaka mitano, yaani The principal of rotating presidency between islands for five years.

Utaratibu huo ulianza vizuri ambako kuanzia mwaka 2002 – 2006 alishika Rais Azali anayetoka Grande Comoro. Mwaka 2007- 2011 urais ulishikwa na Rais Abdallah Mohammed Sambi kutoka Kisiwa cha Anjouan, na mwaka 2012- 2016 Jamhuri ya Comoro iliongozwa na Rais Dk. Ikililou Dhoinine kutoka Kisiwa cha Moheli.

Mwaka 2008 wakati Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa AU, Kisiwa cha Anjouan kilifanya jaribio la kujitenga na visiwa viwili vingine; jambo ambalo Umoja wa Afrika ulilikataa. Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kibali cha Umoja wa Afrika lilikwenda kuzima jaribio hilo kwa kumwondoa kiongozi muasi Kanali Mohamed Bacar na kukirejesha kisiwa hicho kwenye utawala wa Jamhuri ya Comoro. Operesheni hiyo iliyojulikana kwa jina la ‘Operesheni Comoro’ iliongozwa na Brigedia Jenerali Chacha Igoti.

Mwaka 2017 Rais Azali aligombea tena urais na akashinda. Kipindi chake kilikuwa kiishe mwaka 2021 lakini mwaka 2018 akafanya mabadiliko ya katiba bila kushirikisha wananchi na Bunge. Akafuta kipengele cha mzunguko wa urais kwa visiwa wa miaka mitano mitano. Matatizo yalianzia hapo.

Wananchi wakapinga, na Rais mstaafu Sambi akatoa kauli ya kulaani uvunjaji huo wa katiba. Kitendo hicho ndicho kilichosababisha akamatwe na kuwekwa kizuizini kuanzia Mei 18, 2018 hadi sasa.