Watu watatu wamefariki dunia na wengine watano wamejeruhiwa katika ajali ya barabarani eneo la Mogitu wilayani Hanang mkoani Manyara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi, amesema ajali ya kwanza ilihusisha magari mawili ya mizigo, hali iliyofanya barabara isipitike kwa urahisi na kusababisha ajali nyingine eneo hilo hilo, ikihusisha basi la abiria la Kampuni ya Arusha Express, lililokuwa likitokea mkoani Kagera kuelekea Arusha.

Akifafanua amesema baada ya magari hayo ya mizigo yote aina ya Scania kusababisha ajali, polisi wa usalama barabarani waliendelea kuongoza magari mengine yapite kwa utaratibu, lakini ndipo basi hilo lenye namba za usajili T 162 AJB, lilipogonga gari ndogo aina ya Toyota Mitsubishi na pikipiki na kusababisha kifo cha dereva wa gari ndogo na wananchi wengine wawili walioenda kushuhudia ajali ya kwanza.

By Jamhuri