Mkurugenzi Mtendaji wa Hospita ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amezigeukia Yanga, Simba, Azam FC na Coastal Union, kuzingatia zaidi vipimo makini kwa wachezaji wapya watakaowasajili kwa msimu wa 2024/25.

Kauli hiyo ameitoa leo Juni 10, 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwezo wa Hospitali  ya Taifa Muhimbili -Mloganzila, katika tukio la kuagana na nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ambaye alikuwa akifanyiwa matibabu kwenye hospitali hiyo baada ya upasuaji wa goti.

Prof. Janabi amezitaka klabu hizo ambazo zinaenda kuwakilisha nchi katika michuano ya kimatifa, Yanga na Azam FC wakicheza Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Coastal Union wakicheza Kombe la Shirikisho, kuwekeza zaidi katika suala la kupima afya za wachezaji wanaowasajili kwa kuangalia maeneo makuu mawili ambayo ni utimamu wa afya ya magoti na moyo.

“Hizi klabu zinatumia fedha nyingi sana kusajili wachezaji hao wa kigeni, kabla ya kuwapa mkataba wanalazimika kuwapima afya zao, Mlonganzila tupo tayari kuangalia afya za wachezaji hao wanaowasajili.

“Mfano upo hivi karibuni tumeona moja ya klabu haikuweza kumtumia mchezaji wake aliyesajiliwa kwa gharama kubwa na kucheza mechi moja au mbili na kukosa msimu mzima,” amesema Profesa huyo.

Amesema viongozi wa klabu hizo wasidanganyike na ‘Clip’ za YouTube wanazotumiwa kuangalia wachezaji wao kwa ajili ya kuwasajili na kutakiwa zaidi kuwapima afya, ikiwemo magoti na vipimo vya moyo.