Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kisarawe

Mkazi wa kijiji cha Vikumburu Wilayani Kisarawe ,mkoani Pwani, Daud Juma, amejeruhiwa na mapanga katika sehemu mbalimbali za tumbo lake na kikundi cha vijana walioambatana na Mwenyekiti wa kijiji hicho Ramadhan Chaka wakidai anaingilia wanawake bila ridhaa yao kwa mtindo wa kishirikina (Popobawa) .

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dk. Fredy Shayo amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi huyo akitokea kituo cha afya Chole huku.

Hata hivyo alieleza, kutokana na hali ya majeruhi anaendelea kupatiwa matibabu.

Akielezea juu ya tukio hilo lilivyotokea majeruhi ambae amelazwa hospital ya Wilaya ya Kisarawe , Daudi Juma amefafanua kwamba siku ya tukio alikuwa kwenye kibanda chake shambani na ndipo alitokea mwenyekiti na kikundi cha vijana wengi wao wanafahamika.

“Nilipoona hivyo nilishika panga , Mwenyekiti akaniambia niweke panga chini na nikae chini ,akaniambia wewe unadaiwa ni mbakaji, nikashtuka na kusimama nikawaambia mimi sijawahi kubaka ghafla wakaanza kunipiga na mapanga tumboni, nikaanguka chini baada ya kuona hivyo wakaondoka.

“Baadae nilipata nguvu nikakimbilia kwa jirani, nikachukua boda na kukimbizwa Chole hospital,laiti kama nisingeinuka kujinusuru nisingekuwepo hapa sahizi “alijieleza Daud.

Kwa upande wake mdogo wa majeruhi Baisi Masinga amebainisha, mwenyekiti alikuwa na vijana zaidi ya kumi na kufanya msako wakimtafuta mtu anaedaiwa kuwa anakwenda kwa wanawake kisha anawatisha na kuwaingilia kimwili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ,Pius Lutumo akizungumza kwa njia ya simu amekiri kutokea tukio hilo .

Kutokana na mwenyekiti huyo kushindwa kutumia nyadhifa yake kudhibiti kikundi hicho,!” Jeshi la Polisi limemkamata kwa ajili ya uchunguzi .

Amesema, wamepokea taarifa ya mtu mmoja kujeruhiwa, kulikuwa na uvumi kuwa mtu huyo mwanaume anapitia wenzake kwa mtindo wa popobawa yaani kwa imani za kishirikina.

Lutumo amefafanua, uvumi huo uliwaingia watu wachache wakaanza kumtafuta na walipompata wakamshambulia huku mwenyekiti akiwepo pasipo kuzuia, kudhibiti wala kuchukua hatua yeyote hadi polisi walipoenda.

Kutokana na hilo, Jeshi la Polisi limemkamata mwenyekiti huyo ili atoe ushirikiano kwa kosa la kushambuliwa kijana huyo .

Lutumo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wawe wanatoa taarifa kwenye vyombo vya kisheria kwa kwa hatua zaidi.

By Jamhuri