Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

MWENYEKITI wa Kijiji cha Chikola Kata ya Mpwayungu Emanueli Mazengo, Machi 30, mwaka huu, saa saba usiku, aliwakamata wezi waliokata nguzo ya umeme wa masafa marefu kwa msumeno na kuisafirisha kwa Trekta Na T 870 AJA (pichani), ambapo kitendo hicho wamedai, ni kama kumchokoza tena Naibu Waziri Mkuu Dk. Dotto Biteko.

Trekta lililosaidia hujuma ya Nlnguzo hiyo ya umeme, linamilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mpwayungu Festo Manjechi, ambapo Cosmas Chibwana ambaye alikuwa na Pikipiki iliyochomwa Moto na Wananchi wenye hasira, na Asheri Sarah Dereva wa Trekta liliokolewa na Mazengo lisichomwe ndio wanaotuhumiwa

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, Wananchi wa Kijiji hicho wamedai, Cosmas na Asheri walipoulizwa baada ya kukamatwa na nguzo, walijitetea mbele yao kwamba, wameagizwa na uongozi wa CCM Kata, na kwamba tukio hilo ni kama kumchokoza na kukwamisha tena juhudi za Naibu Waziri Mkuu Dk. Biteko anayepambana na hujuma za uharibifu wa vifaa na miundo mbinu ya TANESCO.

“Awali Kijiji chetu kiliibiwa kwa hila mifuko ya Saruji 100 na Matofali yetu na mmoja wa vigogo wa Kata yetu ambapo Mwalimu aliyehusika na wizi wa Saruji hiyo ya Shule alitoroshwa bila kulipa deni letu la nguvu kazi ya wananchi. Kigogo huyo huyo tena amehusika kama alivyoumhadaa mwalimu. Leo tumechoka tumeamua kufanye kweli!”. alisema mmoja wao.

Hivi karibuni Naibu Waziri Mkuu Dk. Biteko alikasirishwa na hujuma, uharibifu na Wizi wa Nyaya, Transfoma na Mafuta yake ambavyo ni Mali ya Umma (‘TANESCO’) zikiwa na gharama ya Mamilioni ya fedha, na kuagiza Menejimenti ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa miundo mbinu Usafirishaji na Usambazaji (ETDCO) ifumuliwe na Bodi yake ivunjwe.

Akijibu tuhuma za waharifu hao na Washirika wao kwa uongozi wa CCM Kata ya Mpwayungu, Mwenyekiti Shadrack Jackson Masinga amesema.

“Hizo ni lugha za mfa maji ambaye kwa vyovyote anajua atazama na kufa!. Ieleweke mafanikio ya kunaswa kwa waharifu hao wa mali za umma (TANESCO), ni juhudi za interejensia ya CCM Kata. Mwizi siku zake ni 40 nazo tayari zimefika ili kuzijua Choroko Mawe ndani ya Chama maana zina rangi”.alisema.

Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Mpwayungu Asheri Juma Msalali alisema, “Kufichaficha Chakula ni kumnenepesha Panya kuliko Paka! Mtu anayekichafua chama kwenye kata, aelewe kuwa wananchi wenye chama chao wakiongzwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Chikola Mazengo, watawashughulikia na kuwaumbua!”.alisema Msalali.

Uongozi wa Tanesco kupitia kitengo cha Usalama kimeshukuru wananchi hao kwa kulinda na kujali rasilimali zao wakiongonzwa na mwenyekiti wa Kijiji hicho, ambapo wamewapongeza Sungusungu na Mbwa wa wasukuma siku moja kabla wizi huo waliwakurupusha wezi hao na kushindwa kufanya uharibifu zaidi wa miundombinu ya TANESCO.

Jeshi la polisi mkoani Dodoma limethibitisha kukamatwa kwa Trekta hilo lililohusika katika kuhujumu miundombini (Nguzo) hiyo ya Tanesco, ambapo linasema linaendelea kufanyia uchunguzi na kwamba Mmiliki wa Trekta hilo Mwenyekitu wa Kata ya Mpwayungu Festo ameachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Uongozi wa Kata hiyo kulikozua sintofahamu kwa wananchi wakidai wanabebana.

Aidha imedaiwa, Watuhumiwa waliohusishwa na Wizi wa Nguzo hiyo wameanza kufanya Njama na kumtishia Mwenyekiti wa Kijiji cha Chikola Mazengo aliyeongoza Sungusungu na Wananchi kuwakamata waharifu hao na Trekta, kwamba watamuwekea Meno ya Tembo ili akamatwe afungwe.

“Tunamuomba Naibu Waziri Mkuu Dk. Dotto Biteko, amlinde Mwenyekiti wetu kwa sababu waharifu hao wanapanga Njama za kumdhuru na kumbambikizia Kesi hiyo kiongozi wetu, kwa sababu amefanikisha kukamatwa kwao, kulinda na kutunza rasilimali za Nchi”.wananchi hao wameomba.