Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MHITIMU wa fani ya udaktari ambaye ni mdogo kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert kairuki (HKMU), Ahlam Azam Mohamed, ametoa siri ya namna alivyofanikiwa kuhitimu akiwa na miaka 21.

Akizungumza na Nipashe jana mara baada ya mahafali ya 21 ya chuo hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Ahlam amesema alimaliza darasa la saba akiwa na umri wa miaka 13 na baada ya hapo hakuendelea na masomo ya darasani.

Amesema baba yake alikuwa akimletea walimu wa masomo mbalimbali nyumbani ambao walimfundisha kwa miezi hiyo minne na kumudu kufanya mtihani wa kidato cha nne katika shule ya Almuntazir kama mtahiniwa binafsi.

“Nilisomea nyumbani masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne kwa miezi minne kisha kikasoma masomo ya kidato cha tano na sita ndani ya mwaka mmoja kwa hiyo nilimaliza masomo ya kidato cha sita nikiwa na miaka 15,” amesema.

“Nilijaribu kujiunga na vyuo lakini majibu yalichelewa kwa hiyo nikalazimika kusubiri mwaka mzima nikaja kujiunga na masomo ya udaktari hapa Kairuki mwaka 2018 nikiwa na miaka 16 na nafurahi leo hii nimehitimu udaktari,” amesema.

Alisema alivutiwa kusomea nyumbani baada ya kumuona kaka yake amefanikiwa kusoma masomo hayo ya kidato kwanza hadi cha nne akiwa nyumbani na kufaulu kwenye mitihani yake.

Awali, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla, alisema chuo kinaona fahari kwa mara ya kwanza kuwa na mhitimu mdogo wa fani ya udaktari kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.

Alisema mhitimu huyo Alham Azam Mohamed alijiunga na chuo hicho mwaka 2018 ambapo amekuwa akifanya vizuri zaidi kwenye masomo yake yote na kufanikiwa kupata Shahada ya udaktari.

“Tulijaribu kupekua pekua kwenye maeneo mbalimbali nchini kuangalia kama kwenye vyuo vya wenzetu hapa nchini kuliwahi kuwa na mhitimu wa fani ya udaktari mwenye umri kama huu lakini ilionekana kwamba mbali na HKMU, hapa nchini huyu ni wa kwanza,” amesema.

Kwenye mahafali hayo, wahitimu walikuwa 308 ambapo mhitimu mmoja alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Sayansi yaani Doctor of Science (Honoris Cause), 13 Stashahada ya Ustawi wa Jamii, 82 Stashahada ya Uuguzi, 14 Shahada ya Ustawi wa Jamii, 35 Shahada ya Uuguzi, 150 Shahada ya Udaktari wa Binadamu.

Wahitimu wawili walitunukiwa Shahada ya Uzamili ya udaktari wa binadamu katika tiba ya afya ya watoto, watatu Shahada ya Uzamili ya Upasuaji, watatu Shahada ya Uzamili ya Magonjwa ya wanawake na uzazi na sita Shahada ya Uzamili ya Tiba.

By Jamhuri