Na Abel Paul,Jeshi la Polisi- Arusha

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kanda ya kaskazini (TMDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha iliendesha operesheni maalum ya kuwasaka watu wanaojihusisha na uzalishaji wa dawa bandia ambapo mamlaka hiyo imefanikiwa kubaini kiwanda bubu ambacho kinatengeneza dawa bandia za mifugo aina ya vidonge maeneo ya Murieti jijini Arusha.

Akiongea na waandishi wa HabarI Mkaguzi wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba kanda ya kaskazini Dkt.Furaha Nyunza amesema wamefanya operesheni hiyo kutokana na uwepo wa dawa bandia zinazoingizwa sokoni kinyume na taratibu za uuzaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini.

Amesema opersheni hiyo imefanyika nchi nzima huku ikihusisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama ambapo ilipelekea kubaini uwepo wa dawa bandia katika maeneo tofauti hapa nchini na kiwanda bubu kinachotengeneza dawa hizo kilichokamatwa maeneo ya Murieti Jijini Arusha.

Dkt Nyunza amebainisha kuwa Uchunguzi umeonyesha kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikitengeneza dawa pasipo kusajiliwa ambapo amewataka wazalisha wa ndani ya kufuata taratibu za usajili wa viwanda vya uzalishaji wa dawa katika mamlaka ya dawa na vifaa tiba hapa nchini.

Aidha amebainisha kuwa operesheni hiyo ni endelevu huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka ya dawa na vifaa tiba kwa kutoa taarifa za watu wawache wanaofanya uzalishaji wa dawa katika mazingira ambayo wanamashaka nayo ili mamlaka hiyo ifanye chunguzi kubaini kama wanazalisha dawa kwa kufuata taratibu.

Ametoa wito kwa watengenezaji wa dawa kutengeneza bidhaa salama kwa watumiaji huku akiwataka kufanya usajili wa viwanda vyao katika mamalaka ya dawa na vifaa tiba ili kutoingia katika mkono wa dora kwa kukiuka taratibu za uzalishaji dawa husika.

By Jamhuri