Immaculate Makilika na Faraja Mpina, JamhuriMedia,Arusha

Mkoa wa Arusha unatazamiwa kuwa Kitovu cha Wataalamu wa Sekta ya Posta barani Afrika mara baada ya uwepo wa jengo la kisasa la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) litakalozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnano Septemba 2, 2023.

Akizungumza jana jijini humo, Mkuu wa Mawasiliano na Itifaki kutoka Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Bw. Faustine Oyuke amesema kuwa Umoja wa Afrika umejenga jengo hilo kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Posta inaboreka na kukuza uchumi wa kidijitali.

“Vilevile ni kuhakikisha jengo hili linakuwa kitovu cha taaluma ya Sekta ya Posta kwasababu kuna ukumbi maalum wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa wataalamu wa Sekta ya Posta barani Afrika ambao ni nchi wanachama na marafiki wa umoja huo ili kuja kujifunza kwa namna gani sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo barani Afrika.”, amesema Bw. Oyuke.

Oyuke amefafanua zaidi kuwa katika jengo hilo kutakuwa na Ofisi za Umoja wa Posta Afrika ambazo zitakuwa katika ghorofa tatu za 13, 14 na 15, Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Kaskazini.

Pia jengo hilo linatajwa kuwa na kumbi za kisasa za mikutano, migahawa ya kisasa na maeneo kwa ajili ya huduma za kifedha.

Kuelekea uzinduzi wa jengo hilo kunatarajiwa kuwa na vikao na mijadala mbalimbali ambapo kesho tarehe 29 Agosti 2023 kutakuwa na kikao cha 41 cha Baraza la Utawala la PAPU, tarehe 31 Agosti 2023, Mjadala wa Biashara wa Posta na tarehe 1 Septemba , 2023 Mkutano wa Mawaziri.