Na Mwandishi Wetu, Jeshi la Polisi-Dar es Salaam

Askari wanawake watakiwa kuwa mstari wa mbele katika kushiriki misheni za kulinda amani katika mataifa yenye changamoto za kiusalama.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya 23 ya adhimio la 13-25 ambalo linalenga kuwashirikisha askari wanawake katika misheni za ulinzi wa Amani.

Akiongea katika maadhimisho ya 23 ya ulinzi wa amani yaliyofanyika katika Chuo Cha taifa cha ulinzi Tanzania kunduchi jijini Dar es salaam Mwakilishi wa UN women Tanzania Bi.Hodan Addou amesema lengo la umoja wa mataifa ni kuwashirikisha askari wanawake katika misheni za ulinzi wa Amani ambapo amebainisha kuwa katika misheni za ulinzi wa amani kumekuwepo na changamoto kubwa kwa makundi ya wanawake na watoto.

Ameeleza kuwa wahanga wakubwa katika machafuko ya kiusalama yanapotokea ni wanawake na watoto huku akisema umoja wa mataifa utaendelea kuweka mazingira bora ya kiusalama kwa makundi hayo.

Kwaupande wake kamishina wa utawala na rasilimali watu wa Jeshi la Polisi CP Suzan Kaganda amesema changamoto kubwa iliyokuwepo Siku za nyuma kwa askari wanawake ni uthubutu na utayari wa ushiriki wa askari wa Kike katika ulinzi wa amani ambapo amebainisha kuwa kwa sasa askari wanawake wamekuwa wakishiriki misheni za ulinzi wa amani kutoka na elimu na kupata kipaumbele na mafunzo ya ulinzi wa amani.

Kwa upande wake balozi wa Swizerland Didier Chassot amesema katika maswala ya ulinzi wa amani lazima waangalie usawa wa kijinsia ili misheni hizo ziwe na matokeo chanya kwa makundi yote huku akiwaomba kuendelea kuweka mazingira bora ya misheni za kulinda amani.

Kwa upande wa uongoz wa kituo cha mafunzo ya ulinzi wa amani umesema umeongeza nafasi za udahili kwa askari wanawake katika mafunzo ili kuongeza uwakirishi wao katika misheni mbalimbali za umoja wa mataifa.