Sisi sote tunatarajia vyombo vya  habari na mchango wake wa Taifa letu. Kwa jumla vyombo vya habari hufanya kazi  tatu. Huelimisha, huchochea maendeleo na huburudisha. Lakini pia vyombo vya habari hupunguza tatizo la ajira. Hutoa ajira.

Mwananchi wa kawaida hunufaika sana na vyombo vya habari. Anaelimika na anachochewa kimaendeleo, anaburudika, na anaweza kupata ajira.

Kwa upande wa kwetu Tanzania Taifa halinufaiki vya kutosha na uhuru mkubwa  wa vyombo vya habari uliopo nchini. Viongozi hawafanyii kazi  habari zinazotolewa na vyombo vya habari. Wanavipuuza.

Kabla hatujazungumzia kwa undani viongozi na Serikali kwa jumla  inavyovipuuza  vyombo vya habari, tuangalie historia ya vyombo vya habari katika nchi yetu angalau kwa kifupi.

Tanganyika (Tanzania Bara) ilianza na magazeti. Kwa miaka mingi wananchi wa Tanganyika  na wa Afrika kwa ujumla hawakuyaamini magazeti. Kila kitu kilichoandikwa gazetini kilipuuzwa. Kilionekana ni uzushi. Watu waliposomewa jambo lolote kutoka gazetini walizoea kusema kwamba hayo ni mambo ya magazeti.

Magazeti  Tanganyika yalianzia mwaka  1888 wakati  wamisheni wa Kanisa  la Kwanza la Anglikana nchini (Magila,Tanga) walipotoa gazeti la “Msimulizi.” Gazeti hili lilisimulia masuala ya elimu. Liliaminiwa na lilipendwa. Hizo zilikuwa enzi za utawala wa Mjerumani. Wakati wa utawala wa Mwingereza, Serikali  ilianzisha gazeti la “Mamboleo” Mwaka 1923.

Gazeti la ‘Mamboleo’ liliwavutia zaidi washairi. Kulikuwa na ukurasa mzima wa mashairi. Wakatokea  washairi maarufu walioendelea  kuandika mashairi yao katika gazeti hilo, miongoni mwao ni Shaaban Robert, Abushiri Mbwana, na Mohamed Chipukizi.

Mambo mengine yaliyoandikwa  katika gazeti  la ‘Mambo Leo’ hata kama yalikuwa  ya kweli yalisaidia  kuwathibitishia wananchi  kwamba magazeti ni uzushi  mtupu. Kwa mfano, safari moja gazeti la “Mambo Leo” liliandika kwamba  mti uliokuwa umeanguka miaka mingi nyuma ulikutwa umesimama!

Wakati wa Vita ya Pili  ya Dunia ya mwaka 1939 hadi 1945, Serikali ilianzisha  gazeti la “Habari za vita.” Wakati ule Tanganyika  ilikuwa imepeleka askari  wake 92,000 nje ya nchi kwenda kupigana upande wa Mwingereza Ethiopia, Somalia, Misri, Uyahudi, na Burma,  kwa hiyo wananchi walifuatilia hali ya ndugu zao vitani kwa kusoma gazeti  la “Habari za vita ” lililotolewa bure.

Gazeti la “Habari za Leo” lilichangia sana katika kuwafahamisha kwamba gazeti huandika uzushi mtupu. Kwa mfano, gazeti liliandika kwamba  askari wa upande wa Mjerumani waliokufa vitani ni 100, litaandika kwamba waliokufa upande wa Muingereza ni wawili!

Katika mazingira hayo watu waliendelea kusema  kwamba hayo ni mambo ya magazeti, ni  uzushi. Baadaye mwaka 1950 Kanisa Katoliki lilianzisha  Gazeti la “Kiongozi” lililokuwa gazeti la dini, liliaminiwa sana. Lilitolewa Kiwanda cha kupiga chapa cha Kipalapala, Tabora. Mhariri wake wa muda mrefu alikuwa Padre Kabeya, aliliendesha gazeti hilo kwa umakini wa hali ya juu.

Mwaka 1952 Dar es Salaam ilipata gazeti la kwanza la kila siku. Liliitwa “Mwangaza”. Gazeti hili liliwavutia sana wakazi wa Dar es Salaam  kwa sababu liliandika  mambo ya kweli yaliyokuwa  yakitokea maeneo yao. Baada ya hapo yalianzishwa magazeti  ya “Baragumu” na “Mwafrika”.

Gazeti la “Mwafrika” lilianzishwa wakati wa kudai harakati za uhuru zilizoongozwa na Chama cha TANU. Gazeti hilo lilipendwa na liliaminiwa sana na wananchi kwa sababu lilishiriki kikamilifu katika kudai  uhuru wa Tanganyika. Kwa upande mwingine, Serikali ya Mwingereza Tanganyika iliona gazeti la “Mwafrika”  kuwa ni la uzushi na uchochezi.

Ukafika mwaka 1958 kipindi cha mapambano makali  ya kisiasa Tanganyika. Gazeti la “Mwafika” likathubutu kuandika kwamba “Mwingereza  asiwadanganye wananchi  kwamba yupo Tanganyika kwa lengo la  kuwastaarabisha wakati yupo hapa kwa lengo la kuwanyonya.”

Wahariri wawili wa gazeti hilo, Rashid Baghdelleh wa Kilwa na Robert Makange  wa Tanga, wakakamatwa. Wakaletwa Mahakama ya Kivukoni, wakahukumiwa kifungo cha miezi sita Gereza la Ukonga. Siku walipotoka gerezani walipokewa kishujaa  katika mapokezi yaliyoongozwa na Chama cha TANU.

Kitendo cha Serikali ya Mwingereza  kuwafunga wahariri wake kwa madai  kwamba waliandika uzushi wakati walikuwa  wameandika ukweli mtupu liliwapa mwanga. Wananchi walijifunza kwamba ukweli kuwa  uzushi kwa yule anayeguswa  na ukweli huo.

Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipata uhuru. Chama cha TANU kilisherehekea siku hiyo kwa kutoa  gazeti la “Uhuru”.

Mwaka 1967 Chama cha Taifa cha Wafanyakazi kilichoitwa NUTA (kifupi cha maneno ya Kiingereza National Union of Tanganyika  Workers) kilianzisha gazeti la wafanyakazi  lililoitwa “Mfanyakazi”.

Mwaka  1972 TANU ilianzisha gazeti la kila Jumapili lililoitwa “Mzalendo”. Basi kabla ya Tanzania kuingia  kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 magazeti  maarufu ya Kiswahili  yalikuwa Kiongozi, Mfanyakazi, Uhuru na Mzalendo.

Magazeti hayo yote yalijitahidi kuandika ukweli mtupu katika kipindi  hicho ambacho hakikuwa  na ushindani mkubwa wa kisiasa, kilikuwa kipindi cha chama kimoja. Magazeti yalipoandika ukweli kuhusu  kiongozi fulani, uongozi ulikuja juu. Kesho yake alidai kuwa mwandishi wa habari alikuwa amemnukuu vibaya.

Mwingereza enzi zake, mbali na kuanzisha gazeti la “Mambo Leo” mwaka 1923, alianzisha Kituo cha Redio mjini Dar es Salam Mwaka 1951. Kituo hicho  cha redio kilianzishwa mtaa wa Kichwele (miaka hii Mtaa wa Uhuru) jirani kabisa na Kiwanda cha Bia, kiliitwa Sauti ya Dar es Salam kwa sababu redio ilisikika  Dar es Salam tu.

Mwaka 1954  kituo cha Sauti ya Dar es Salaam kilihamishiwa Barabara ya Pugu (Barabara ya Nyerere) na kiliitwa Sauti ya Tanganyika kwa sababu redio ilisikika kote  Tanganyika. Wananchi walinufaika na vipindi vya burudani kama michezo ya kuigiza, mashairi, na vichekesho pia  kwa kupelekeana salamu  zilizoandamana na muziki motomoto.

Baada ya kuingia  mfumo wa vyama  mwaka 1992, Tanzania  haikupata vyama vingi tu. Pia ilipata vyombo vingi vya habari  ikiwa ni pamoja  na magazeti  redio na runinga. Japokuwa hapa si mahali pake si vibaya tukizungumzia kwa kifupi Tanzania inavyonufaika na mfumo wa vyama vingi. Upinzani umesaidia kwa kiasi kikubwa chama tawala na Serikali yake kuendelea kuwa macho ili visinyang’anywe madaraka yake ya utawala.

Lakini Tanzania ingeweza kufanya vizuri zaidi kama ingetumia vizuri zaidi mfumo wa vyama vingi. Kilichotokea ni haki ya kuonekana waziwazi chama tawala na vyama vya upinzani. Kwa mfano, chama tawala  kitatangaza  kuwa kitanuia  kutoa elimu  bure. Chama  cha  upinzani  kitainuka na kudai  kuwa chama tawala  kimeiba sera yake. Katika mazingira hayo hapana shaka vyama vya upinzani vimeficha sera zao  mifukoni ikihofia kuwa sera hizo zitaibwa na chama tawala.

Vyama vya upinzani vinasubiri kutumia sera zake au mawazo yake mazuri  vikishika madaraka ya utawala japo haijulikani lini. Kwa upande mwingine, Tanzania ina utaratibu mzuri wa kushirikisha vyama vya upinzani kwenye masuala ya Bajeti ya Serikali. Katika mkutano wa Bunge la Bajeti mawaziri halisi na mawazili vivuli (wa kambi ya upinzani) hutoa mawazo yao kuhusu utekelezaji  wa shughuli za sekta  mbalimbali za Taifa.

Haijulikani Serikali inatumia kwa kiasi gani  mchango wa vyama vya upinzani,  utakuta Serikali inaepuka kutumia mawazo  mazuri ya vyama vya upinzani kwa kuhofia kwamba ikitumia mawazo hayo wapinzani wataaminiwa na wananchi  na watapewa kura wakati wa uchaguzi. Ni ubinafsi tu unaodhoofisha  maendeleo ya Taifa.

Sisi sote tunajua nchi zilizopata maendeleo makubwa duniani na zile  zilizotumia vizuri mfumo wa vyama vingi, ukiweka kando nchi za kikomunisti. Tusije tukaendelea kujivunia mfumo wa vyama vingi ambao haunufaishi sana Taifa letu. Turudi upande  wa vyombo vya habari unakuta kwamba uhuru wa vyombo vya habari  ulioshamiri Tanzania haunufaishi sana Taifa letu mbali na kuwaelimisha, kuwaburudisha na kuwachochea  wananchi kimaendeleo.

Tumebaki kuwa na sifa tu kwamba tuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari huku Serikali ikishindwa kutumia vizuri uhuru huo kwa maendeleo ya Taifa, kila mtu anajua kwamba Serikali inatumia mamilioni ya shilingi za umma kununua magazeti ya kila haina kwa ajiri ya mawaziri  wake na maofisa wake mbalimbali.

Huwezi kukuta lundo kubwa la magazeti ofisi za Serikali. Ukweli ni kwamba ni viongozi wachache sana wa Serikali  wanaofanyia kazi  yanayoandikwa magazetini. Wengi wanaendelea kuyaangalia magazeti kama vyombo vya uzushi na uchochezi. Kuna magazeti ambayo yana safu maalum ya kuandika kero za wananchi. Lakini nani anajali!

Katika nchi zilizoendelea, kama Uingereza na Marekani, huwezi kukuta gazeti limeandika kashfa nzito  inayomhusu waziri au kiongozi yeyote wa Serikali  au Shirika la Umma, kesho ikawa kimya. Serikali itafuatilia mara moja kashfa hiyo  kwa lengo la kujisafisha au kuchukua hatua kali dhidi ya mhusika.

Kwetu Tanzania mambo ni tofauti kabisa, waziri anaandikwa weee! mpaka magazeti  yanachoka yenyewe Serikali iko kimya. Viongozi watawasiliana kwa simu na kuchekeshana kutokana na hayo yaliyoandikwa gazetini  kana kwamba hayawaathiri wao wenyewe, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Pengine hapa ni vyema tukizungumzia athari za Serikali za kupuuza magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla. Kwanza, heshima ya mhusika inapungua mbele ya umma. Na kama kiongozi wa Serikali pia heshima ya Serikali inapungua.

Pili, kashfa ambayo inamhusu mtu mmoja isiposhugulikiwa huhusishwa  na viongozi wengine. Watu huona kiongozi mhusika  analindwa kwa sababu anachofanya hakimnufaishi peke yake. Wanasema wanakula naye.

Tatu, kwa kuwa kiongozi anayefanya maovu  hachukuliwi hatua  anaendelea kufanya maovu tena  makubwa zaidi. Nne, magazeti hufika mahali yanachoka kufichua maovu, kwa hiyo maovu yanaongezeka. Tano, tusije  tukasahau kwamba  magazeti yetu yanasomwa na wageni na majirani zetu wanapoendelea kusoma kashfa  ambazo hakuna anayeshugulikia  na sisi tumesifika kwa utawala bora, bila ya shaka wanatushangaa, wanatucheka, na wanatudharau.

Sita, mbele ya wananchi na mbele ya wageni  Serikali inaonekana ni dhaifu. Nani  anaheshimu Serikali dhaifu? Saba, wananchi wanapoteza  kabisa imani juu ya Serikali yao. Kila mtu anajua  matokeo ya wananchi kupoteza imani  juu ya Serikali yao. Wanajitenga na chama tawala na Serikali yake wanaungana  na vyama va upinzani.

Chukua kwa mfano, ubabe wa Serikali iliyodumu mikoa ya Lindi na Mtwara  kwa miaka miwili ambapo wananchi wameendelea kusumbuliwa na jeshi lao la ulinzi  na wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara. Viongozi wa mikoa wakiwamo chama tawala waliendelea kulalamika kupitia vyombo vya habari. Lakini hakuna aliyejali.

Niliwahi  kuandika katika gazeti hili  kwamba kwa miaka mingi mikoa ya Lindi  na Mtwara imekuwa ngome ya kutegemewa  ya Chama Cha Mapinduzi. Nikaishauri Serikali itumie busara katika kushughulikia matatizo ya gesi kule kusini. Hata Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwahi kuitaka Serikali iwasikilize wananchi wa kusini. Lakini nani alijali. Nilionya kwamba Serikali ikiendeleza ubabe wake  kusini wananchi watakikimbia chama tawala. Nilichoandika ndicho kilichotokea.

Majuzi wakati wa ziara  ya Mwenyekiti  wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, wanachama wote wa CCM Kijiji cha Lihanga, Mtwara, wamejiunga na CUF. Anguko la CCM  halisababishwi na vyama  tawala na Serikali yake. Lakini dalili ya mvua ni mawingu. Hiyo mvua iliyonyesha majuzi Mtwara inaweza kuwa mvua ya rasharasha tu. Mvua zenyewe za masika zitanyesha wakati wa uchaguzi  wa Serikali za Mitaa na chaguzi zitakazofuata  baada ya hapo.

Sisi sote ni mashahidi  unapofika wakati wa uchaguzi tumezoea  chama tawala kikijigamba  kwamba Serikali yake ni sikivu  na inashugulkia vyema  kero za wananchi.

Hakuna asiyekubali kwamba Serikali imefanya kazi nzuri  katika kushughulikia kero za wananchi. Lakini ingeweza kufanya  vizuri zaidi kama isingepuuza  vyombo vya habari. Serikali imeshindwa kutumia vizuri  uhuru mkubwa wa vyombo  vya habari uliopo nchini. Sasa ikabili athari zake.

By Jamhuri