MOMBASA

NA DUKULE INJENI

Kampeni za kisiasa nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mapema mwezi ujao zinaingia hatua za lala salama huku kila upande ukitumia vema majukwaa ya siasa kupigana vijembe badala ya kuuza sera.

Licha ya uwapo wa wagombea urais wanne waliopitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ni wawili tu ndio wanaonekana kuwa na ushawishi na wamekuwa wakichuana vikali katika utafiti wa kura za maoni zinazotolewa na taasisi mbalimbali.

 Ni dhahiri kuwa sasa atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta na kuwa Rais wa tano wa Kenya ni ama Naibu Rais William Ruto au aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

Ruto anawania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilicho katika Muungano wa Kenya Kwanza wakati Odinga anawania urais kupitia Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Wagombea wengine wa urais kuelekea uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 9, 2022 ni Profesa George Wajackoyah wa Chama cha Roots anayeshinikiza kilimo cha bangi ili kutumika kuleta fedha za kigeni na David Mwaure wa Chama cha Agano.

Kwa mujibu wa utafiti wa kura za maoni uliotolewa hivi karibuni, umaarafu wa Ruto umepungua kiasi kwamba kama uchaguzi ungefanyika wakati huu, Raila angeshinda japo kwa asilimia ndogo, kwani watu ambao hawajaamua wampigie nani kura bado ni wengi.  

Miongoni mwa sababu zilizosababisha umaarufu wa Ruto kupungua ni kauli zake za hivi karibuni zinazoonyesha ni kiongozi mwenye jazba, hivyo kuwapa hofu wapiga kura kwamba huenda akawa rais mwenye hasira.

Kanda ya sauti imevuja ikisikika Ruto akisema nusura amzabe kofi Uhuru aliyetaka kuweka pembeni azima yake ya kuwania urais kwa muhula wa pili mwaka 2017 baada ya Mahakama ya Upeo (Supreme Court) kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi ya IEBC yaliyompa Uhuru na Ruto ushindi.

Ruto anasema wasingekubali juhudi walizozifanya kuhakikisha Chama cha Jubilee kinapata ushindi katika uchaguzi huo wa 2017 zinapotea kisa Uhuru anataka kususia jina lake kuwamo katika masanduku ya kupigia kura.

Uhuru anajibu sauti hiyo ya kanda kwa kukiri ni kweli alitaka kujiweka pembeni na kurudi zake nyumbani kutokana na  uamuzi wa mahakama kufutilia mbali ushindi wake, lengo likiwa ni kuepusha umwagaji wa damu.

“Kama wangenipiga kofi kwa sababu ya madaraka, ningewapa shavu la pili wanipige kofi. Ndiyo, nilitaka kurudi Ichaweri (kijiji anachotoka Uhuru) kwa sababu nisingeweza kulinganisha madaraka na umwagaji wa damu,” anasema Uhuru.

Baadaye ilifahamika si tu Uhuru ambaye nusura azabwe kofi na Ruto ila pia Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa, anadai kidogo atandikwe kofi mwaka 2018 baada ya kukerwa na kitendo chake cha kuchukua viongozi wa jamii yake kukutana na Uhuru baada ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Kauli hii ya Wamalwa na ile sauti iliyosikika ya Ruto zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa wa Muungano wa Azimio la Umoja kuwashawishi wapiga kura watafanya makosa kumchagua Ruto kwa kuwa ni mtu mwenye hasira.

Aidha, wamekuwa wakihoji kama anadiriki kutaka kumzaba kofi Rais wa nchi nini anachoweza kumfanyia mwananchi wa kawaida na hasira alizonazo? Haikupita siku katika moja ya mikutano ya kisiasa Ruto akakatiza hotuba yake na kumfokea mtu akidai anaukosea heshima mkutano wake wa siasa.

“Tuwe na heshima. Kama kuna mtu ametumwa hapa kuja kuharibu mkutano mseme saa hii mapema ama muondoke kwa hii mkutano. Wewe kijana wacha kunijibu, unanijibu kama nani? Kama umeleta kisirani kwa hii mkutano utoke. Huwezi kuja hapa kuharibu mkutano,” anafoka Ruto.

Akitetea hasira zake ambazo wapinzani wake wanazitumia kama turufu, Ruto, anasema inachangiwa na gharama za maisha kupanda na Wakenya hawana furaha kwa sababu nchi inaelekea njia panda.

Ruto anasema hasira dhidi ya gharama ya maisha kupanda itachochea Wakenya kupiga kura kwa serikali makini, yenye maono na inayowajibika ikifika Agosti 9, 2022.

By Jamhuri