Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Lt. Jen. (Mst) Yacoub Hassan Mohamed amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo Mjini Abu Dhabi.

Akizungumza baada ya kupokea hati hizo, Rais Al Nahyan alimuhakikishia Mhe. Balozi Mohamed ushirikiano na Serikali yake katika kutekeleza majukumu yake nchini UAE kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi Mohamed alimuahidi Mhe. Rais kuwa atahakikisha Watanzania na Waemirati wananufaika na fursa za kiuchumi zilizopo katika pande zote mbili.

Tanzania na UAE zina fursa nyingi za kushirikiana kiuchumi hususan katika sekta ya nishati ambayo UAE ni miongoni mwa nchi tajiri katika uzalishaji wa mafuta. Tanzania ina eneo kubwa la kilimo hivyo ina soko kubwa la bidhaa za Kilimo na Mifugo ambapo ushirikiano huo utawezesha uzalishaji wa kisasa na kuongeza thamani ya bidhaa.

Bidhaa zenye soko kubwa kwa Tanzania nchini UAE ni mbogamboga, matunda, nyama, korosho, karafuu, chai, karanga, asali, samaki na kahawa.

Pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu ubalozi huo pia unawakilisha nchi za Bahrain, Pakistan na Iran.