Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge amezielekeza Halmashauri za mkoa huo kuandaa mikakati thabiti itakayoziwezesha kuongeza ukusanyaji mapato ili kuisaidia serikali kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Kunenge ameyasema hayo kwenye kikao kazi maalum kilichofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha cha kuandaa mpango mkakati wa ukusanyaji mapato kwa kipindi cha miaka mitano mkoani humo.

Alisema mpango huo utakuwa ni dira ambayo utaisaidia mkoa wa Pwani kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda, uvuvi, mifugo, kilimo na uchumi wa bluu.

“Ni hatua muhimu sana kwa mkoa wetu katika kuhakikisha tunawahudumia wananchi kupitia rasilimali zetu za ndani, tunahitaji tukusanye mapato katika kila sekta lakini kwa utaratibu mzuri ambao hautawaumiza wananchi wetu, “ amesema Kunenge.

Ameongeza kuwa mkoa wa Pwani umekuwa wa kwanza kujengewa uwezo na Serikali ya watu wa Ujerumani GIZ katika kufanikisha mpango bora wa ukusanyaji mapato na kwamba watahakikisha mkoa huo unakuwa kinara wa mapato nchini.

Aidha, Kunenge amewashauri wakuu wa mikoa wengine nchini kujifunza mbinu za kisayansi za kukusanya na kuongeza mapato na kwamba ofisi yake ipo tayari kutoa uzoefu wake ili kwa pamoja waisaidie serikali kupata fedha za kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon alisema mpango huo wa miaka mitano utasaidia kuongeza ukusanyaji mapato kutoka sh. bilioni moja hadi bilioni 20.

Amesema miongoni mwa vyanzo wanavyovikusudia ni bandari kavu ya Kwala, mradi wa ujenzi wa nyumba na viwanja vya michezo.

“Tunaamini mbinu hizi za kisayansi zitatusaidia sisi Kibaha kuongeza ukusanyaji wa mapato na tupo tayari kulisimamia hili kwani uwezo wa kufanya hivyo tunao kwa sababu tuna rasilimali za kutosha.

Mtaalam Msimamizi wa Fedha za Umma kutoka Serikali ya Watu wa Ujerumani GIZ nchini Tanzania, Eriko Amon anasema kuwa mpango huo utasaidia kuweka utaratibu wa kuwatambua wafanyabiashara, kuchambua maeneo yanayosababisha fedha kukosekana ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Katika kikao hicho, Nsajigwa George aliyemuwakilisha Katibu Tawala mkoa wa Pwani alieleza, mpango huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na dira ya maendeleo ya mkoa huo.

Ameeleza, mkakati huo wa utekelezaji ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na viongozi wa mkoa huo katika kuisaidia serikali kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi.

By Jamhuri