Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Mbambabay

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa David Kihenzile amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 70 kuanza uboresha bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.

Amesema mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo ni miezi 24 na kwamba Mkandarasi amekabidhiwa eneo la mradi Januari 26,2024 na kwamba kukamilika kwa mradi kutaongeza uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo kwa bandari hiyo kutoka tani 110,000 hadi 550,000 kwa mwaka.

“Uboreshaji wa bandari hiyo ni maandalizi ya kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR ukanda wa kusini kutoka Mtwara hadi Mbambabay mkoani Ruvuma na kuunganisha Liganga na Mchuchuma mkoani Njombe’’,alisisitiza.

Ameitaja nia ya serikali ni kuhakikisha kwamba reli ya kutoka Mtwara hadi Mbambabay inajengwa na kwamba kazi inayofanywa na serikali hivi sasa ni kuhakikisha inatafutwa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli hiyo.

Amesisitiza kuwa mradi huo utakapokamilika utatoa fursa ya usafirishaji katika ushoroba wa Mtwara na nchi za Maziwa Makuu za Malawi na Zambia.

Kuanzishwa kwa Reli ya kusini itakuwa ni ukombozi kwa mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara kwa kuwa mahitaji ya treni katika huduma ya usafiri na usafirishaji hivi sasa ni makubwa kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo uchimbaji wa makaa ya mawe mkoani Ruvuma.

Historia inaonesha kuwa Katika miaka ya 1950 Mkoani Lindi kulikuwa na reli inayotoka Nachingwea kupitia Mtama, Mnazi Mmoja, Mingoyo hadi Bandari ya Mtwara na ilikuwa ikisafirisha korosho, mbao, magogo na watu.

Naibu Waziri wa Uchukuzi amefanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma ya kukagua mradi wa kiwanja cha Ndege cha Songea,mradi wa uboreshaji wa bandari ya Mbambabay na bandari 15 zilizopo katika ziwa Nyasa.