Kenya imewasamehe walio na pasipoti kutoka nchi saba kulipa ada ya kuingia nchini humo iliyoanzishwa mwezi uliopita.

Serikali ilitupilia mbali mahitaji ya viza kwa wamiliki wote wa pasipoti za kigeni.

Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kuitangaza Kenya kama kivutio cha utalii na kuvutia wasafiri wa kibiashara. Lakini ada ya kuingia ya $30 ilianzishwa, ikijumuisha kwa wageni wengine ambao hapo awali hawakuhitaji visa.

Uamuzi huo ulizua msukosuko mkubwa, huku wakosoaji wakisema kuwa huenda ukasababisha nchi ambazo Kenya ina mikataba ya kuondoa visa kuanzisha ada sawa na hiyo, hivyo kufanya usafiri kuwa wa gharama kubwa na urasimu.

Msamaha huo umeongezwa kwa wenye hati za kusafiria kutoka mataifa sita ya Afrika – Afrika Kusini, Ethiopia, Eritrea, Congo-Brazzaville, Comoro na Msumbiji.

San Marino, taifa la tatu kwa udogo barani Ulaya, ndiyo nchi nyingine pekee kwenye orodha ya kutotozwa ada.