Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa kifo cha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi ni pigo kubwa, si kwa Mkoa huo pekee, bali Chama, serikali na taifa zima kwa ujumla.

Amesema, Wakasuvi amefikwa na mauti akiwa ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo, iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Nchimbi amesema kuwa Wakasuvi alikuwa mmoja wa viongozi shupavu wa CCM, kuanzia mkoani kwake, hadi ngazi ya taifa, ambapo kutokana na uwezo na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na ushirikiano tangu alipochanguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM, mwaka 2007, aliendelea kuaminiwa hadi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, nafasi aliyokuwa nayo hadi mauti yalipomfika.

Nchimbi amesema hayo leo Februari 24, 2024 alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi kwenye mazishi ya Wakasuvi yaliyofanyika katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora yakiongozwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Samia Suluhu Hassan.

“Kiwango cha kuaminiwa Mzee Wakasuvi kilikuwa ni kikubwa sana, mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Mkoa na Mjumbe wa NEC ya CCM Taifa, pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Lakini pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha chetu. Makamu wake alikuwa ni Mzee Wassira (Steven), ” amesema Nchimbi na kuongeza.

” Wanauliza watu maswali mbalimbali, mimi ilikuwa imepangwa niwatembelee na kuonana nao Jumatatu (keshokutwa), wakaniulize maswali waliyopanga kuniuliza nami nilikuwa nimejiandaa kwenda kujibu maswali hayo,” amesema

Amesema, Chama kimepoteza, Serikali imepoteza na Wananchi kwa ujumla wamepoteza kiongozi mahiri na shupavu.