Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono mpango unaopendekezwa na Marekani wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Gaza.

Pendekezo hilo limeweka masharti ya “kusitisha mapigano kamili “, kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, kurejeshwa kwa mabaki ya mateka waliokufa na kubadilishana wafungwa wa Kipalestina.

Wajumbe 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio hilo lililoandaliwa na Marekani. Urusi ilijizuia.

Azimio hilo linasema kuwa Israel imekubali pendekezo la kusitisha mapigano, na kuwataka Hamas kukubaliana nalo pia.

Ina maana Baraza la Usalama linaungana na serikali kadhaa, pamoja na kundi la mataifa tajiri zaidi duniani la G7, katika kuunga mkono mpango wa sehemu tatu ambao ulizinduliwa na Rais Joe Biden tarehe 31 Mei.

Kura hiyo huenda ikaongeza shinikizo kwa pande zote mbili kujibu vyema mpango huo kwa nia ya kumaliza mzozo huo.

Pia hatua hiyo inajiri muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na viongozi wa kigeni, akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika jaribio la kujenga uungwaji mkono kwa mpango huo wa amani.

Saa chache kabla ya kura ya Umoja wa Mataifa, Bw Blinken alisema ujumbe wake kwa viongozi katika eneo hilo ulikuwa: “Ikiwa unataka kusitishwa kwa mapigano, washinikize Hamas waseme, ndiyo.”

By Jamhuri