Watumishi wasisitizwa Umoja, Upendo na Ushirikiano

Dkt. Budeba awaasa watumishi kuwa wawazi

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba ameongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la taasisi hiyo uliyofanyika leo Januari 14, 2024 katika ukumbi wa Prof. Abdulkarim Mruma Jijini Dodoma.

Akifungua Mkutano huo, Dkt. Budeba ameanza kwa kuwaasa watumishi wote na wajumbe wa Baraza hilo kushiriki kikamilifu kwa kuwa wawazi na kutumia fursa hiyo kuwasilisha na kujadili hoja muhimu zitakazopelekea uboreshaji na ufanisi wa majukumu ya taasisi hiyo.

“Kila mtumishi azungumze hoja kwa uwazi bila kuwa na hofu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika maeneo yetu ili kuleta umoja, upendo na mshikamano hususan katika kipindi hiki cha Vision 2030, “Madini ni Maisha na Utajiri”.

Kwa upande wake, Mchumi Mkuu wa GST Lameck Kajala amewasilisha mada ya mapito na mchanganuo wa Bajeti ulioidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mwaka 2023/24 na Rasimu ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

Naye, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Mkoa wa Dodoma (TUGHE) Samwel Nyungwa amesema Balaza la Wafanyakazi lipo kwa mujibu wa Sheria ambalo ni agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 ambalo kazi zake ni pamoja na kuishauri serikali katika shughuli zake na kuhakikisha watumishi wa serikali wanashirikishwa kwenye shughuli za kiserikali.

Katika Mkutano huo watumishi na wajumbe wote wamepata fursa ya kujadili utejelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kujadili na kupitisha Rasimu ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kwa manufaa ya taasisi hiyo.