Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge amezindua mradi wa kilimo cha Pamba wilayani Rufiji utakaotekelezwa na Kampuni ya Rufiji Cotton Ltd ambapo pia amepokea matrekta na pikipiki zitazotumika kwenye mradi huo.

Akizungumza na wananchi wa Chumbi kwenye uzinduzi huo, aliwapongeza wawekezaji hao kutoka India kwa uwekezaji huo.

Ameeleza kuwa kwenye historia ya Pamba ilianza kulimwa nchini kwa mara ya kwanza wilayani Rufiji mwaka 1964 hivyo Serikali ipo tayari kuumpa ushirikiano mwekezaji huyo.

“Kwenye kipaumbele changu kwa Mkoa Kilimo ni kipaumbele na bado hakijafanya vizuri, “wilaya ya Rufiji kwa kuendelea kuwapokea wawekezaji kwa sasa wilaya hii ina wawekezaji wakubwa wa Kilimo cha Sukari, na Kilimo cha Pamba, niwaombe wakazi wa Rufiji kutumia fursa hizi mnazopata”alieleza Kunenge.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Wille Mtunga alieleza kuwa ,ziara ya India ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imezaa matunda na tunazindua mradi wa Pamba Rufiji.

Anaeleza kwa historia Pamba ilianza kupandwa Wilaya ya Rufiji, wamepita vijiji 24 wilayani Rufiji kufundisha juu ya kilimo bora cha pamba.

Alisema, ili kuwa na kilimo bora wameleta timu ya ushindi ambao ni maafisa ugani 24 watakao hudumu kwenye vijiji hivyo 24.

“Mpaka sasa tumesajili wakulima wenye jumla ya ekari 3012 wilayani Rufiji, ifikapo wiki ijayo tutaaleta mbegu za pamba, viutilifu, mabomba ya kupulizia mazao na vyote vitagawiwa kwa wakulima bure.”

Balozi wa zao la Pamba Nchini ,Aggrey Mwanri, ametuma Salaam kwa Rais Dkt Samia za pongezi kwa kuvutia uwekezaji katika sekta ya Pamba.

Alieleza kuwa kilo zinazozalishwa wilayani Rufiji ni laki moja na kiwanda kitakacho jengwa kitahitaji kilo laki tano.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Rufiji Cotton Ltd ,Hassan Kinje alieleza , wamekuja kuwekeza Rufiji kwa sababu ya mazingira mazuri ya uwekezaji, kampuni itatoa uwezeshaji wa huduma bure ya matrekta kwa ajili ya kilimo.

Vilevile wameajiri maafisa ugani 24 na kutoa pikipiki ambazo zitatumika kutoa elimu kwa wakulima na wanategemea kujenga kiwanda cha kuchambua Pamba, kiwanda vya nguo.

Kwa upande wake, Ally Athuman Nguyu Diwani kata ya Chumbi alipongeza
Wananchi kujitolea ekari 6000 kwa ajili kilimo cha Pamba na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata pamba.