Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Njombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuzilinda tunu za umoja wa kitaifa za utulivu, amani  na ushirikiano. 

Rai hiyo ametoa wakati akimwakilisha Mheshimiwa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika Misa ya kuweka wakfu Askofu wa Jimbo la Njombe Dkt. Eusebius Samwel Kyando iliyofanyika Mkoani Njombe tarehe 14 Januari, 2024.

Waziri amesema kuwa tunu hizo ndizo zinazotambulisha  Taifa letu la Tanzania duniani na ulimwenguni kote.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu )  Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi zawadi Mhashamu Askofu Dkt. Eusebius Kyando mara baada ya Misa ya kuwekwa wakfu.

“Tunu hizi zilindwe kwa kuzingatia umuhimu wake, pia Serikali inashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa, tunaomba muendelee kuliombea bila kuchoka ”  alifafanua Waziri 

Aidha  viongozi wa dini mmekua mstari wa mbele kuhakikisha Taifa hili linaendelea kuwa katika hali ya utulivu mstahimilivu na Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele Kati Jambo hilo.

“Niwaombe Sana Viongozi wa dini tuendelee kukemea pale tunapoona kuna viashiria vya watu wachache kuvunja amani, utulivu umoja na mshikamano wa Nchi yetu,” alihimiza

Aidha aliitaka jamii kuungana na Serikali katika kupaza sauti juu ya matendo maovu na hasa mauaji na ukatili wa kijinsia, imani potovu ambazo zinapelekea mauaji na unyanyasaji wa watoto wadogo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu )  Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mhasham Askofu Damian Dalu wa Jimbo la Songea, mara baada ya ibada ya kuwekwa wakfu Askofu wa Jimbo la Njombe.


Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka ameomba viongozi wa dini kwa kushirikiana na serikali kwa pamoja kuunga mkono jitihada zinazofanywa katika sekta ya elimu hasa katika masuala ya lishe kwa wanafunzi mashuleni katika  kukabiliana na tatizo la utapiamlo.

“Hii itasaidia kuleta hamasa kuwaandaa watoto kwa  kuwapatia lishe Bora ambayo itawasaidia kufanya vizuri katika maisha yao,”
Alisema.

Kwa upande wake mmoja wa waumini wa kanisa hilo Bi, Naomi Nzota amesema waumini wa Jimbo la Njombe wamefurahi Sana  kwa kupata Askofu Dkt. Eusebius Kyando baada ya Misa wa kuweka wakfu iliyoongozwa na Muasham Askofu Mstaafu wa Jimbo la Dar es salaam Polcapy Pengo.

“Ameueleza utumishi wa  Askofu Dkt. Eusebius Kyando kwamba ni mtumishi, mnyenyekevu mnyoofu na mvumilivu,” alieleza.

Waumini mbalimbali waliojitokeza katika Misa ya kumuweka wakfu Askofu wa Jimbo la Njombe Mhashamu, Dkt. Eusebius Kyando iliyofanyika katika Mkoa wa Njombe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu )  Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka wakiwa katika picha ya pamoja na Mhashamu Askofu Dkt. Eusebius Kyando mara baada ya Ibada ya kumweka wakfu askofu huyo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)*