Barua ya wazi kwa Rais kuhusu wamachinga

DAR ES SALAAM

Na Sabatho Nyamsenda

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,

Natumaini u-buheri wa afya. Karibu tena nyumbani baada ya kutoka Marekani ulikohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA). 

Natumaini umefurahi kurejea nyumbani. Shaaban Robert alighani akisema: “Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa.” Naam! Nyumbani ni nyumbani, alituimbia Remmy Ongala.

Bila shaka utakuwa umeona jinsi hotuba yako kwenye mkutano wa UNGA ilivyosifiwa katika vyombo vya hapa nyumbani. Natamani ningeifanyia uchambuzi, lakini pengine hilo ni jambo la siku nyingine. 

Nilitaka kukuuliza swali: Je, umeyaonaje mazingira ya Dar es Salaam ulipotoka ‘airport’ kwa gari kuelekea Ikulu? Bila shaka wasaidizi wako wamekwambia ‘jiji’ limeanza kuwa safi baada ya kubomoa vibanda vya wamachinga eneo la Vingunguti. 

Bila shaka wamekueleza kuwa ndani ya wiki tano zijazo, Mkoa wote wa Dar es Salaam utakuwa safi kama Vingunguti! Wasaidizi wako wanasema wamefanya hivyo kwa ajili yako – eti kwa kuwa unaitangaza Tanzania ipate watalii wengi, ni aibu watalii wakishuka uwanja wa ndege na kuelekea katika hoteli zao wakaona uchafu! 

Na uchafu huo si takataka bali ni watu – wamachinga – na bidhaa wanazouza.

Azima hiyo ya kuifanya Dar es Salaam kuwa safi tena (twaweza kuiita MADCA, yaani Making Dar es Salaam Clean Again) ilitangazwa na Amos Makalla mara tu ulipomteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

‘Mzaliwa wa Dar’ huyu, kama anavyojiita, alitangaza operesheni ya kuwaondoa wamachinga kutoka katikati ya jiji huku akiomba viongozi wakuu wamvumilie maana anakwenda ‘kuwafinya’ watu. 

Alitoa sababu kadhaa kwa nini anawaondoa wamachinga: kusafisha jiji, maana wamachinga wamechafua jiji; kupunguza ajali za barabarani, maana wamachinga wameziba njia za magari na watembea kwa miguu; kuleta taswira ya jiji, maana biashara haziwezi kufanyika kila sehemu; kuokoa uhai wa wamachinga, maana wanafanya kazi katika mazingira hatarishi; na sababu nyingine nyingi.

Katika mahojiano na vyombo vya habari na hotuba zake kadhaa, Makalla amekuwa akionyesha kukerwa na uwepo wa wamachinga katikati ya jiji huku akitolea mfano wa jinsi inavyoharibu taswira ya jiji kumwona mama ameweka jiko na sufuria lenye masizi akipika ugali pembeni ya barabara iliyojengwa kwa bei ghali! 

Katika fikra za Makalla, mama huyo anapaswa kutimuliwa na kupelekwa pembezoni ili asichafue taswira ya jiji na kuwakimbiza watalii. Sababu yoyote itatolewa ili kuhalalisha kumwondoa mmachinga huyo anayeuza maji, chakula, nguo au matunda. 

Kinachofanyika hivi sasa ni mbinu ambayo Waingereza wanaiita; ‘give a dog a bad name in order to hang him’, yaani kumpatia mbwa jina baya ili kumnyonga.

Uzushi mwingi umetungwa kusema kuwa mama ntilie, yaani mama lishe, wanapikia chini ya transifoma za umeme utafikiri maeneo yote ya katikati ya jiji yamejaa transifoma na hakuna mahali palipo salama! 

Ikiwa kuna mitambo ya umeme, itatumiwa kama kisingizio cha kumwondoa mmachinga hata kama pembeni ya mitambo hiyo kuna hoteli kubwa (kama ilivyo Landmark Hotel) au kituo cha mabasi (kama ilivyokuwa stendi ya daladala ya Ubungo kwa miongo kadhaa kabla ya kuhamishiwa Mawasiliano) au hata ofisi za serikali (kama zilivyokuwa ofisi za TANESCO pale Ubungo).

Wapo wengi, hasa wafanyabiashara wakubwa na wa kati pamoja na wasomi, wanaompongeza Makalla. Wamachinga walio wengi wanamlaani, wakisema wazi kuwa anawarudisha katika zama za giza ambapo walikuwa wakipigwa, kuporwa bidhaa zao, kuswekwa ndani na kunyimwa haki ya kuwapo katika jiji. 

Wengine wamekwenda mbali na kuuliza: je, kuna uhusiano gani kati ya Makalla na kuungua masoko ya wamachinga? Kwa nini akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya liliungua Soko la SIDO na kwa nini alipokuja Dar es Salaam likaungua Soko la Kariakoo? Mambo haya yanaweza kuwa ni ya kupangwa (design) au yakawa yametokea kwa nasibu (coincidence) tu. 

Unavyo vyombo vya uchunguzi, nafikiri vinaweza kukusaidia kufuatilia. Jambo lililo wazi ni kuwa Makalla anawachukia wamachinga. Chuki hizi sidhani kama zinatokana na roho mbaya au kukosa utu. Nataka kuamini kuwa Makalla, licha ya dharau, ubabe na majigambo yake dhidi ya wamachinga, ni mtu mwenye utu.

Tatizo, nionavyo mimi, lipo katika mtazamo unaomwongoza Makalla katika kulitazama jiji na watu wake, ambao ndio wenye walakini. Mtazamo huo, Mheshimiwa Rais, haujaanzishwa na Makalla na hautamalizika naye. 

Kiini chake ni sera za kikoloni za mipango miji na dola la kinyapara tulivyorithi kutoka kwa wakoloni. Tokea makao ya serikali yalipohamishiwa Dar es Salaam na wakoloni wa Kijerumani kutokea Bagamoyo, na sera hiyo kuendelezwa na Waingereza, mji wa Dar es Salaam ulipangiliwa katika kanda tatu kulingana na hadhi ya uraia. 

Ukanda wa kwanza ulikuwa Uzunguni, ambapo waliishi Wazungu ambao walikuwa raia wa daraja la kwanza, ukifuatiwa na ukanda wa pili ulioitwa Uhindini, ambako waliishi watu wenye asili ya Asia, ambao walikuwa raia wa daraja la pili. Uswahilini, waliishi wenyeji, Waafrika ambao hawakuhesabika kama raia (citizens) bali watawaliwa (subjects).

Uswahilini kulikosa huduma za kijamii na miundombinu, na kadiri mji ulivyopanuka, Waswahili walisukumwa pembezoni zaidi. Leseni za biashara zilitolewa kwa Waasia/Wahindi ambao ndio walikuwa kiungo kati ya Wazungu na Waafrika, huku Waswahili wakibaki kuchuuza vijibidhaa na kuviuza katika vijibanda vyao. 

Historia ya Dar es Salaam inaonyesha kuwa Kariakoo ilikuwa eneo la Uswahilini ambalo lilistawi kwa vijibiashara vya uchuuzi vya Waafrika/Waswahili, ambavyo hata hivyo havikuhesabika kama shughuli halali ya kujipatia kipato.

Kwa kuwa dola la kikoloni lilikuwa na kazi ya kutumia mabavu ili kuwakalia Waafrika kwa lengo la kunyonya nguvu-kazi yao na kupora rasilimali zao, basi mara kwa mara liliendesha operesheni za kuwatimua Waafrika kutoka mijini ili warejee vijijini, likiwaita ni wahuni (hooligans). 

Mamlaka hayo ya timua timua walikabidhiwa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, kwa kushirikiana na vyombo vya mabavu kama polisi.

Baada ya uhuru kupatikana, sera zetu za mipango miji na mifumo yetu ya utawala viliendelea kufuata misingi ile ile ya ukoloni, hivyo kudurufisha mfumo wa utawala wa kinyapara na mipango miji ya kikoloni isiyozingatia mahitaji ya walio wengi. 

Si ajabu kwamba sera za timua timua za wamachinga na matabaka ya watu maskini kama watu wasio na ajira, ombaomba na wapiga debe zimeendelea katika awamu zote hapa nchini, isipokuwa Awamu ya Tano baada ya kiongozi wake kuamua kubadili mwelekeo.

Mheshimiwa Rais, mtazamo wa mtangulizi wako, Dk. John Magufuli, ambaye ulifanya naye kazi kama makamu wake, ulijikita katika dhana ya haki-jiji (right to the city) kwamba watu wa matabaka ya chini (kama wamachinga) wana haki ya kujipatia kipato katikati ya jiji, na kunapotokea mgongano kati ya haki-jiji za wamachinga na mambo mengine, basi haki-jiji za wamachinga zipewe kipaumbele. 

Ukizungumza na wamachinga watakwambia kwamba katika kipindi cha kuanzia Juni 2016 hadi Machi 17, 2021 ndicho kipindi ambacho walijisikia watu huru, ambao utu wao ulithaminiwa na mali zao ziliheshimiwa.

Mheshimiwa Rais, uliporithi mikoba ya urais kutoka kwa Magufuli uliahidi kuendeleza mambo mema aliyoyafanya, hasa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa Bwawa la Nyerere na reli ya SGR, na ulisema wazi kuwa serikali yako ikishindwa kuiendeleza miradi hiyo mtapata laana. Wengi tulifarijika kusikia kauli hizo kutoka kwako. 

Hata hivyo, miradi ya ujenzi itaacha urithi wa vitu, ambayo yaweza kuwa sura moja tu ya maendeleo – maendeleo ya vitu. Sura ya pili ya maendeleo ni maendeleo ya watu, kupitia sera zinazojali na kuheshimu utu wao, pamoja na kuboresha ustawi wao. Sura hizi mbili zinapaswa kufungamanishwa kwa sababu bila kuzingatia maendeleo ya utu, basi maendeleo ya vitu yatapoteza maana.

Katika kitabu chake cha ‘Binadamu na Maendeleo’, Mwalimu Julius Nyerere ametolea mfano vitu, kama piramidi za kustajaabisha za Misri na barabara nzuri za Urumi, ambavyo licha ya ukubwa, uzuri na umaarufu wake, viliachwa vijiozee kwa sababu havikuwa na maana katika utu na ustawi wa walio wengi. 

Wanajeshi wa kigeni wa Urumi waliitelekeza dola hiyo ilipovamiwa na kuacha barabara zake nzuri kama ambavyo watumwa waliojenga piramidi za Misri walivyokimbia na kuacha utamaduni wake uanguke. Haya yote ni kwa sababu barabara na piramidi hayo hayakulenga katika kutunza utu wao na kuboresha ustawi wao.

Japokuwa utawala wake ulikuwa na upungufu katika baadhi ya maeneo, hasa katika matumizi ya mabavu kukabiliana na upinzani, Rais Magufuli alijitahidi sana ilipokuja kwenye suala la kusimamia haki za wamachinga, wachimbaji wadogo, na hata jamii za wafugaji na wakulima wadogo. 

Na kama vile alikuwa akijitabiria kifo chake, Magufuli alikuita Ikulu wewe na wawakilishi wa TAMISEMI Desemba 6, 2016 na kukuambia kuwa hafurahishwi na namna ambavyo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wanavyowafukuza wamachinga kutoka katikati ya jiji na kuwapeleka maeneo yasiyo na biashara!

Magufuli aliweka msimamo kuwa kiongozi yeyote ambaye hayuko tayari kuwaona wamachinga wakifanya shughuli zao bila bughudha katikati ya jiji, basi ajiuzulu mara moja. 

Baada ya kifo chake ndipo wengi wetu tumegundua kuwa alikuwa akikupatia wosia, kwamba ikitokea akafariki dunia, basi uwatunze ‘yatima wake’. Leo hii wateule wako wanawakejeli wamachinga kuwa haki zao zilizikwa Chato; kwamba yatima hadeki. 

Kama ambavyo umeikwepa laana ya kutelekeza miradi mkakati ya SGR na Bwawa la Nyerere, ndivyo hivyo hivyo ninakusihi uikwepe laana ya kuwadhulumu wamachinga haki yao ya msingi ya kufanya biashara katikati ya jiji.

Mheshimiwa Rais, kama unavyofahamu, pamoja na kulinda haki-jiji katika uwanda wa kisiasa, Rais Magufuli hakuweza kwenda mbali kwa kuzitafsiri haki-jiji katika mfumo wa kisera na kisheria. Jambo hilo ndilo ninaloshauri uongozi wako ulifanye. 

Nashauri kuwe na mageuzi makubwa ya kisera na kisheria kwa upande wa mipango miji pamoja na mfumo wa kidola ili kutoa haki kwa zaidi ya robo tatu ya wakazi wa mijini ambao wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi. Baadhi ya hatua ambazo ninashauri uanze nazo ni:

    (a) Kusitisha amri ya kuwahamisha wamachinga kutoka maeneo ya katikati ya miji nchini kote, ukianzia na Dar es Salaam.

   (b) Kufanya uchunguzi kuhusu operesheni za kuwatimua wamachinga zilizosababisha zahama katika maeneo ya Mchikichi/Msimbazi na Vingunguti Scania jijini Dar es Salaam, ambazo zina viashiria vya rushwa, ufisadi, uporaji wa mali za wamachinga, matumizi ya nguvu yanayosemekana kusababisha majeraha kwa wamachinga na hata kifo cha mtu mmoja katika eneo la Vingunguti, na kufunguliwa mashitaka kwa wamachinga na kiongozi wao mmoja katika eneo la Mchikichi/Msimbazi. 

Je, ni kwa nini wafanyabiashara wakubwa wawili ambao ni ndugu ndio waliomwongoza mkuu wa mkoa katika ziara yake ya Kariakoo na mmoja wa wafanyabiashara hao ndiye anayetumia nguvu, ikiwamo kuajiri mabaunsa kuwapiga wamachinga, kuharibu mali zao na kuwafukuza katika eneo la hifadhi ya barabara iliyopo mbele ya duka lake?

    (c) Kuomba msamaha na kutoa fidia kwa familia za wamachinga waliopoteza maisha na kujeruhiwa kutokana na kadhia ya bomoa bomoa ya Vingunguti; wamachinga 177 wa Vingunguti walioporwa bidhaa zao kupitia bomoa bomoa; na  wamachinga 18 waliopoteza vyanzo vyao vya maisha katika eneo la hifadhi ya barabara mbele ya duka la Sandaland, Kariakoo. 

Kufanya hivyo ni uungwana na kurejesha faraja na imani kwa waathirika wa vitendo vinavyosemekana kufanywa na mamlaka za kidola na wafanyabiashara wakubwa.

    (d) Kupitia upya sera na sheria za mipango miji ili kuondokana na kiini cha ukoloni katika mipango miji na ujenzi wa miundombinu. Badala yake dhana za ‘majiji jumuishi’ (inclusive cities) na ‘haki-jiji’ (right to the city) zitumike katika kubuni upya ujenzi wa barabara, vituo vya daladala na mabasi, na mpangilio wa miji unaozingatia matamanio na mahitaji ya walio wengi. 

Kwa mfano, kuna ubaya gani kuongeza mita mbili kila upande katika barabara kwa ajili ya wamachinga? Pia, maeneo ya hifadhi ya barabara ambayo hayatumiki yaruhusiwe kutumiwa na wamachinga. Kadhalika, badala ya kuwahamisha wamachinga katika maeneo yenye msongamano, uangalie uwezekano wa serikali kununua baadhi ya majengo katika maeneo hayo ili kutanua eneo linalotumiwa na wamachinga, au kufunga baadhi ya barabara ili mitaa hiyo ibaki kuwa mitaa maalumu ya wamachinga.

    (e) Haya yote yatawezekana iwapo kutakuwa na ushirikishwaji wa kweli wa wamachinga katika maeneo waliyopo. Ushirikishwaji ni lazima ufanyike kwa uwazi kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe katika eneo lao walilopo, na lengo lisiwe kuwahamisha bali kuwapa nafasi wajipange wenyewe katika eneo walilopo na kutoa maoni juu ya nini cha kuboresha.

Nakushukuru, Mheshimiwa Rais, kwamba uliona uwezekano wa matumizi ya mabavu kuwaondoa wamachinga ndiyo maana ukaagiza kuwa, mosi, hautaki kuona matumizi ya nguvu katika kuwaondoa wamachinga, na pili, wamachinga wapangwe. 

Ukweli ni kwamba mabavu yametumika kwa aina mbili: moja kwa moja katika uvunjaji, uporaji na upigaji wa wamachinga, pia katika utoaji wa amri za kuhama pasi na kuwashirikisha wamachinga. 

Dhana ya kupangwa imetumika kama mbinu ya kuwaondoa wamachinga katika maeneo yenye mzunguko wa watu ili kuwapeleka maeneo maalumu bila ridhaa yao. 

Ukweli ni kwamba licha ya matumizi ya mabavu, hamisha-hamisha hii haitazaa matunda zaidi ya maumivu na uporaji, hivyo kuitia doa serikali yako. Mwishowe, hata baada ya kusababishiwa hasara na maumivu, wamachinga watarudi tu katika maeneo yale yale ya awali bila kujali hasara watakayoipata kwa sababu hawana mbadala.

Tusisahau kuwa serikali za awamu ya tatu na ya nne zilikuja na dhana za kuvutia za ujenzi wa maghorofa kama Machinga Complex kwa ajili ya kuwapeleka wamachinga. Cha kushangaza, wamachinga waliishia kupanga bidhaa zao barabarani, nje ya maghorofa hayo na kukataa kabisa kuhamia ghorofani. 

Kulikuwa na ulazima gani kutumia mabilioni ya fedha kujenga masoko ya maghorofa ambayo walengwa wamegoma kuyatumia? Hawakushirikishwa: mipango ilibuniwa na kutekelezwa bila kuzingatia mahitaji ya umachinga.

Laiti wamachinga wangeulizwa, wangewafafanulia wataalamu wa mipango miji kuwa umachinga kwa asili yake ni tofauti na biashara ya soko la kawaida au duka. 

Mmachinga hutembeza bidhaa zake kumfuata mteja au hupanga bidhaa zake mahali palipo na mzunguko wa watu (kama vituo vya daladala) ili zionwe na kununuliwa. 

Mabilioni yaliyoteketezwa kujenga maghorofa yaliyo tupu yangeweza kutumika kutanua maeneo yanayozunguka vituo vya daladala pamoja na kuchonga meza ili wamachinga wapange bidhaa zao katika maeneo yenye watu.

Mheshimiwa Rais, bila shaka utakuwa umeambiwa kuwa wamachinga walio wengi ni matajiri sana, hivyo wamejaza makontena na mafriji barabarani. 

Jihadhari na uongo huu unaoenezwa na baadhi ya watawala, akiwamo ‘mzaliwa wa Dar’. Unaongoza nchi maskini, ambayo watu wake walio wengi ni mafukara wa kutupwa.

Japo kuna matabaka ndani yao, wamachinga walio wengi ni maskini sana, wenye mtaji usiofika Sh 100,000. Watu hawa walipaswa kupewa ruzuku ya kuwawezesha kuishi na serikali, pamoja na kupata huduma za kijamii bila malipo. Lakini serikali haifanyi hivyo. 

Njia njema ni kutowanyang’anya hata hiyo nafasi finyu ya kujipatia kipato katikati ya jiji, japokuwa kipato chenyewe hakitoshelezi hata kuwapatia chakula, achilia mbali mahitaji mengine ya msingi.

Mheshimiwa Rais, unaongoza nchi yenye uchumi legelege, unaosafirisha ajira kwenda ughaibuni kwa mfumo wa malighafi na kuingiza umaskini kwa mfumo wa bidhaa zilizozalishwa nje. Uchumi huo legelege hauzalishi ajira zenye staha; unazalisha umaskini kwa walio wengi. Katika watu wapya milioni moja wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka, wanaoajiriwa katika sekta rasmi ni 40,000 tu. 

Sehemu kubwa ya watu 960,000 wanaobakia, hulazimika kujihusisha na kilimo au kujihusisha na biashara ya umachinga katika sekta isiyo rasmi. Sehemu kubwa ya wahitimu wetu wa vyuo vikuu nao huangukia katika kundi hili, ambalo hapo zamani lilikuwa ni la watu wenye elimu ya chini pekee.

Kwa hiyo, umachinga ni dalili ya ugonjwa wa uchumi wetu legelege usiozalisha ajira zenye staha. Tatizo la umachinga haliwezi kuondolewa kwa kuwaadhibu wamachinga, kama ambavyo umaskini hauwezi kuondolewa kwa kuwaadhibu watu maskini. 

Umachinga unaweza kupunguzwa kwa kujenga uchumi uliofungamanisha sekta za viwanda na kilimo ili uchumi wetu usisafirishe ajira nje ya nchi. Lakini yapo masharti ya ujenzi wa uchumi wa aina hiyo, ambayo ukipenda nitayafafanua zaidi katika barua yangu nyingine.

Mheshimiwa Rais, kama umefanikiwa kuisoma barua hii, nina uhakika umeanza kuchoshwa na urefu wake, japokuwa ningetamani kukuandikia juzuu kadhaa za kitabu kufafanua hoja zangu, huku nikitolea mifano ya nchi kadha wa kadha. Lakini ngoja nikomee hapa. 

Nakuachia dhana tatu, ambazo ndizo kiini cha barua yangu: jiji jumuishi (inclusive city), haki-jiji (right to the city) na uchumi unaojiendesha (self-sustaining economy). 

Ukiweza kuzifanyia kazi vilivyo utaacha alama ya dhahabu katika mioyo ya walio wengi, alama itakayoishi milele na kusimuliwa kizazi hata kizazi. Kinyume cha hapo, utaacha doa litakaloacha simulizi za majuto na ukatili.

Haki-Jiji sasa inawezekana, Mheshimiwa Rais. Kupanga ni kuchagua.

Mwandishi amejitambulisha kuwa ni Mtanzania na Mwana wa Afrika. Makala hii imechapwa kwa ruhusa ya tovuti ya www.udadisi.com