DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Kukinzana na kugongana kwa taratibu na sheria kati ya idara mbili nyeti za serikali kumesababisha wataalamu saba kutoka nje ya nchi kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili, wataalamu hao saba waliletwa nchini na Kampuni ya Saruji Tanga (Tanga Cement), kwa ajili yakutoa mafunzo kwa wafanyakazi raia wa Tanzania.

Kuwapo nchini kwa wataalamu hao kutoka Afrika Kusini, kumegonganisha sheria na taratibu za Idara ya Uhamiaji na Idara ya Kazi mkoani Tanga, baada ya Idara ya Kazi kuwakamata na kuwafungulia mashitaka.

Ofisa Masoko na Mawasiliano wa Tanga Cement, Mtanga Noor, amelieleza JAMHURI kuwa si mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuwaleta nchini wataalamu kutoa mafunzo ya ukarabati wa mitambo ya kuzalisha saruji na klinka.

“Lakini ajabu Septemba 6, mwaka huu, maofisa wa Idara ya Kazi Mkoa wa Tanga walifika kiwandani na kuwachukua na kwenda kuwahoji Kituo cha Polisi Chumbageni,” anasema Mtanga. 

Mtanga anasema kampuni ilifuata taratibu zote za Uhamiaji kuhakikisha hakuna usumbufu utakaowapata, ikiwamo vibali kwa ajili ya ‘kazi maalumu’.

Vibali hivyo ni maalumu kwa wafanyakazi ambao si waajiriwa rasmi kufanya kazi kwa muda usiozidi miezi mitatu.

“Tanga Cement inaendeshwa kwa weledi mkubwa na kwa kufuata sheria zote za nchi ndiyo maana inaaminika katika utendaji wake,” anasema.

Mtanga anawataja wataalamu hao saba kuwa ni Francois Kleyn mwenye kibali namba 0062818, John Pienaar (0062815), Keith Randall (00062998), Charles Albert (00062817), Jan Andries Van Der Westhuizen (00062691), Wayne Van Niekerk (0062822) na Charles Thoneson (00062692).

JAMHURI linafahamu kwamba wataalamu hao waliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, wakapatiwa vibali (business visa) na Idara ya Uhamiaji na kutimiza masharti yote ya kuingia nchini. 

Vibali kama hivi hutolewa kwa wageni kwa ajili ya kazi maalumu kama kurekebisha mitambao na kuendesha mafunzo maalumu ya muda mfupi na kazi nyingine kwa mujibu wa sheria za Uhamiaji.

“Waliwasili nchini Agosti 9 na 19, mwaka huu, hivyo hawajavusha muda waliopewa na Uhamiaji, yaani miezi mitatu,” anasema.

Kwa nini wamekuja nchini?

Kuhusu sababu za kampuni kuwaleta nchini wataalamu hao, Mtanga anasema wakati taifa lilipokumbwa na uhaba wa saruji katika siku za hivi karibuni, Tanga Cement wakajikuta wakikumbana pia na changamoto ya mitambo.

“Hapo tukalazimika kuwaita wataalamu kuja kufanya ukarabati wa mitambo. Sisi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa saruji nchini, hivyo inapotokea changamoto ya kiuzalishaji au usambazaji, athari yake huonekana wazi. 

“Tukaamua kuleta wataalamu watakaowafundisha wafanyakazi wa Kitanzania ili tatizo kama hilo lisijitokeze tena,” anasema Mtanga.

Baada ya kampuni kununua vipuri kwa fedha nyingi, Mtanga anasema wakalazimika kuwapa kazi ya kuvifunga vipuri hivyo kampuni ilivyovileta.  

“Kwa maana hiyo hawa si waajiriwa wa Tanga Cement ila ni waajiriwa wa Kampuni ya Multi Tegnik ya Afrika Kusini iliyotuuzia vipuri, kisha tukaipa kazi ya kuvifunga na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wetu, huku wakibadilishana utaalamu,” anasema. 

Ni wafanyakazi watano tu miongoni mwa 267 walioajiriwa na Tanga Cement ndio wageni wenye kuhitaji vibali vya Uhamiaji.

Jinsi walivyokamatwa

Septemba, mwaka huu, maofisa wa Idara ya Kazi Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Janeth Omolo, walifika kiwandani hapo kufanya kile kilichoelezwa awali kama ‘ukaguzi wa kawaida’.

Huku Janeth akionekana kupewa maelekezo kwa njia ya simu, anasema Mtanga, akawa akiwataka wenyeji wake kumpeleka idara moja hadi nyingine na kila alipokuta mgeni, alimuamuru kuandamana naye.

“Tukamwambia ni vema tumuitie wageni wote, kwa sababu tunafahamu kuwa wapo kihalali. Wana vibali vinavyowaruhusu kufanya kazi.

“Akawachukua wale wageni wataalamu saba na kwenda nao Kituo cha Polisi Chumbageni, wakatoa maelezo, wakaachiwa kwa dhamana.

“Tukaanza kutafuta miongozo bila mafanikio. Tulikwenda hadi Dodoma kuonana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi akiwa na Kamishna wa Kazi na Ofisa wa Kazi. Tukaelekezwa kurudi Tanga katafuta ufumbuzi,” anasema.

Anasema wamekuwa wakikutana mara kadhaa na Janeth lakini hakuna ufumbuzi uliopatikana. 

Anasema Idara ya Kazi mkoani Tanga inataka wataalamu hao watafutiwe vibali vya kazi, suala ambalo ni kinyume cha sheria na utaratibu. 

“Moja ya mahitaji ya kupata vibali vya kazi ni kuwa na mkataba kati ya mwajiri na mfanyakazi. Hawa sisi si wafanyakazi wetu. Tanga Cement haina mkataba nao wala haijawaajiri wataalamu hawa, hivyo hatuwezi kuomba vibali vya kazi kwa ajili ya watu ambao hatuna mkataba nao wa ajira,” anasema.

Idara ya Kazi, Uhamiaji wagoma kuzungumza

Wiki iliyopita JAMHURI lilimtafuta Ofisa Kazi Mkoa wa Tanga, Janeth Omolo, kujua kwa nini wataalamu hao wamefikishwa mahakamani licha ya kuwa na vibali vya Uhamiaji, na akajibu kwa kifupi:

“Suala lililopo mahakamani siwezi kulizungumzia, tuiache mahakama ifanye kazi yake.”

Kwa upande mwingine, JAMHURI limezungumza na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Petro Malima, kujua sababu za wataalamu hao kukamatwa licha ya kuwa na vibali vinavyodaiwa kuwa ni halali na vimetolewa na Idara ya Uhamiaji.

“Ni vema ukamuuliza mtu wa ‘Labour’ (Idara ya Kazi) kwa sababu (wageni hao) wana vibali vya Uhamiaji. Lakini ukiona ni muhimu kuniona, basi ninaomba tuonane kesho (Jumatano ya wiki iliyopita),” anasema Malima.

Katika hatua nyingine, Tovuti ya Idara ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz) inasema kibali (business visa) kinatolewa kwa raia wa kigeni kuingia nchini kwa madhumuni ya kufanya kazi maalumu kama kukarabati mitambo au kuendesha mafunzo ya muda mfupi.

Pamoja na mambo mengine, pia kufanya kazi za kitaaluma kama uhasibu au kufanya shughuli halali iliyoruhusiwa kisheria huku kampuni inayomleta nayo inatakiwa kuwasilisha nyaraka halali, ikiwamo leseni ya biashara na cheti cha kampuni na mkataba unaoonyesha shughuli maalumu atakazofanya raia huyo wa kigeni.

Hii si mara ya kwanza

Migongano kama hii ya kiidara imekuwa ikitokea mara kwa mara na kuwasababishia usumbufu mkubwa wataalamu kutoka nje pamoja na wawekezaji.

Miaka kadhaa iliyopita wataalamu walioletwa nchini na Kampuni ya uwindaji wa kitalii, Ortello Business Cooperation (OBC), walijikuta wakikamatwa na maofisa wa serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wataalamu hao walidaiwa kufanya kazi bila kuwa na vibali halali, pamoja na ukweli kwamba waliletwa nchini kwa kazi maalumu na ya muda mfupi, ambayo hadi wanakamatwa walikuwa wamekwisha kuikamilisha.

Baada ya mivutano ya kisheria na makubaliano waliachiwa ingawa tayari jina la Tanzania kwa wawekezaji kutoka nje lilikuwa limekwisha kuchafuliwa.

By Jamhuri