Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) kufanya kazi za usanifu wa makaravati na madaraja kwa kuzingatia viwango vya ubora ili yatakapojengwa yaweze kustahimili na kudumu kwa muda mrefu.

Amesema kwa mameneja watakaofanya uzembe na kusababisha hasara, watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua.

Bashungwa alitoa onyo hilo akiwa katika kijiji cha Nguyami, Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro alipokuwa akikagua na kuona eneo litakapojengwa daraja la kudumu katika mto Nguyami na kujionea karavati lililolojengwa awali katika mto huo na kubomoka muda mfupi kutokana na kubaini lilijengwa chini ya kiwango .

Waziri Bashungwa alimwelekeza Mtendaji Mkuu Tanroads, Mhandisi Mohamed Besta kuwa alichokiona kwenye daraja la mto Nguyami hataki kukiona tena popote .

“Hiki nilichokiona hapa kwanza nitafuatilia ni nani aliifanya hii kazi na kulipwa fedha ili tumchukulie hatua na wengine wakajifunge kwa hatua tulizochukua …makaravati yamebomoka kwa muda mfupi na fedha ya serikali imepotea kutokana na uchakachuaji,”

“Hapa fedha zimepotea, sasa nilichokiona hapa Nguyami ole wenu Meneja wa Tanroads nitakapokuja mikoani na nikakuta hali kama hii niliyoiona hapa hata kama umehamishwa mkoa mwingine kule kule nitakufuata nitakutumbua huko huko”. alionya Bashungwa.

Waziri Bashungwa alisema tayari usanifu wa kina umeshafanyika  wa ujenzi wa daraja jipya  ambapo mahitaji yake ni kujengwa daraja la urefu wa mita 100 na lenye viwango vya kisasa.

Alisema kuwa  daraja la kisasa litalojengwa  litaunganisha mawasiliano ya barabara ya Mkoa wa Morogoro kutoka Wilaya ya Gairo na Kilindi Mkoa wa Tanga.

“Nikuelekeze Meneja wa Tanaroads mkoa, usanifu wa kina umeshafanyika na tumeshajua mahitaji ya daraja hili, linahitajika kujengwa daraja la mita 100 , ambalo litaunganisha mawasiliano ya barabara kwa mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Kilindi,Tanga.

Bashungwa alisema kwa sasa hatua inayofuatia ni kufanya manunuzi ya kumpata mkandarasi  na kutaka  jambo hilo lifanyike haraka kabla ya kuhitimishwa mwaka huu wa bajeti inayoisha Juni 30 ili mkandarasi awe amekabidhiwa kuanza kazi mara moja.

Waziri Bashungwa alitaja daraja lingine ni la mto Chakwale ambalo lina urefu wa mita 80 nalo lipo mbioni kujengwa pia  ni kuinganishi cha mawasiliano ya barabara hiyo kwenda Kilindi, mkoani Tanga.

Naye Mbunge wa Jimbo la Gairo, Ahmed Shabiby  alisema mto Chakwale ambako hakuna daraja unapojaa  maji yanachukua muda mrefu kupungua na kukwamisha shughuli za uzalishaji mali .

Alisema mto huo  umeshasababisha maafa mengi ya watu na mali zao vikiwemo vyombo vya usafiri pamoja na mto Nguyami ambao hauna daraja kaa kusababisha zaidi ya magari nane amezama eneo hilo na maafa ya watu.

Shabiby alisema mwaka 2022 serikali kuu ilitoa fedha kiasi cha Sh  bilioni 159 kwa ajili ya usanifu kwa madaraja mawili ya Chakwale na Nguyami

Mbunge hiyo alimwomba Waziri kuwa madaraja yatakayojengwa Chakwale na Nguyami yalingane na kiwango cha barabara ya lami itakayokuja kujengwa.