Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,DODOMA

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini(DCEA) wametoa mafunzo kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano ili kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya .

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jijini hapa ,Kamishna wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema mafunzo hayo yatasaidia kufanikiwa kwa Programu ya TAKUKURU rafiki katika tatizo la dawa za kulevya na mapambano dhidi ya Rushwa kwa maafisa hao na kuleta matokeo chanya.

Amesema elimu ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya ikitiliwa mkazo zaidi mashuleni itasaidia kulinusuru kundi la watoto wenye miaka kati ya 10 hadi 12 ambalo kwa siku za hivi karibuni limetajwa kuwa hatarini zaidi kwenye uraibu wa dawa za kulevya.

“Rushwa na dawa za kulevya zinaingiliana, tumieni mafunzo mliyoyapata kutoa elimu kwa jamii na kuwapa uelewa ili kuongeza chachu ya mapambano na udhibiti wa madawa ya kulevya hivyo,tumeanza kwa wanafunzi ngazi za msingi,sekondari hadi vyuo vikuu hivyo kupitia klabu zao za kupambana na Rushwa watatumia pia klabu hizohizo kupambana na madawa ya kulevya , “amesema

Ameongeza kuwa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) zimeamua kuungana kwani zinafanana katika utendaji kazi wake na kuamua kutokomeza kabisa madawa ya kulevya na Rushwa ambayo ni chanzo kikubwa cha kumaliza nguvu kazi ya taifa ambayo asilimia kubwa ni vijana,kuhakikisha wanatetea nchi kwani haki huinua taifa.

Pamoja na hayo amesema “Rushwa huleta madhara kiuchumi, kimaadili na mnyororo mzima wa uongozi na kusababisha huduma za jamii kudidimia, tunataka kuweka mkazo kwa kuwafikia wanafunzi wote nchini, ” amesisitiza

Katika kutilia mkazo zaidi ameeleza kuwa Taasisi hizo zinaenda kuboresha klabu za wanafunzi shuleni kuungana na kuwa moja itakayoshughulikia kupinga rushwa na madawa ya kulevya jambo litakalosaidia kuleta uelewa wa pamoja na kujenga uzalendo.

“Tukifanya hivi tutakuwa tumeitengeneza jamii inayochukia rushwa kwenye maeneo mengi na kuwaokoa wanafunzi wanaotumika kwenye dawa za kulevya kwa kigezo cha ufaulu na kuwasababishia uraibu,pia itasaidia kuongeza uchumi kwa sababu wawekezaji wanapenda kuwekeza sehemu yenye amani bila rushwa, amesema.

“Ili kufanikiwa haya, tunawapatia miongozo ya utoaji elimu wa namna ya kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu rushwa na dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuwasaidia waraibu kupata tiba saidizi, tutambue kuwa tunafanya kazi ya Mungu kwa kuwarudisha watu watende haki kwa kuikataa rushwa na kurudi kwenye maadili, ” amesisitiza.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye amesema kuwa mafunzo hayo yaliyofanyika siku tatu yamewasaidia maafisa hao namna ya mbinu za kuongeza katika utendaji kazi na hususani katika programu ya kushirikisha jamii katika mapambano ya Rushwa programu mahususi ya TAKUKURU rafiki.

Amesema, “Ni matumaini yetu kwamba mafunzo hayo yataleta matokeo chanya kwa jamii ya kitanzania dhidi ya Rushwa na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya,tunatarajia kuona kiwango cha ushiriki wa wananchi katika kushirikiana na taasisi hizi mbili kikiongezeka,” amesema