*Yeye, wenzake wafungiwa vituo kwa kuchakachua

*Walipa mamilioni ya shilingi


Kampuni ya Lake Oil inayomilikuwa na bilionea Ally Awadh, imeingia matatani baada ya vituo vyake vinne vya mafuta kufungiwa kutokana na kuuza mafuta yasiyokuwa na vinasaba.

Vituo vilivyofungwa ni Lake Oil kilichopo Manzese, Songea; Lake Oil kilichopo Makambako, Lake Oil kilichopo Kisasa mkoani Dodoma, na Lake Oil kilichopo Gairo mkoani Morogoro.

Vituo hivyo ni sehemu ya vituo 18 vilivyopewa adhabu hiyo na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa vituo hivyo vilifungwa wiki iliyopita, wakati wa ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na maofisa wa EWURA. Hata hivyo, kuna habari kwamba Lake Oil wamelipa faini ya Sh milioni 28.

Kwa kawaida, mafuta yasiyokuwa na vinasaba huwa yanasafirishwa nje ya nchi, lakini badala yake yamekuwa yakiuzwa katika soko la ndani bila kulipiwa kodi.

Mmiliki wa Lake Oil, Awadh, alipoulizwa juu ya kufungiwa kwa vituo vyake vinne kutokana na makosa ya kutokuwa na vinasaba, alijibu kwa maandishi, “Nataka kukuhakikishia sitatetereka hata siku moja na hizo blackmail (vitisho) zako.

Pia nitapambana na wewe kisheria hadi napata haki yangu kwa jinsi ulivyonidhalilisha na kunisingizia vitu vya uwongo. I will never negotiate with a fool like you! (Kamwe sitajadiliana na mjinga kama wewe!”

Taarifa hizi zimekuja huku JAMHURI ikiandika habari zinazoihusu kampuni fulani, inayotuhumiwa kukwepa kodi inayofikia Sh bilioni 26 kutokana na biashara ya uuzaji mafuta nchini licha ya udanganyifu unaofanywa kuonesha kuwa yanapelekwa nchi jirani.

Kampuni ya Lake Oil, ingawa haijatajwa kwenye habari hiyo, imejitokeza na kusambaza matangazo yenye thamani ya mamilioni ya shilingi katika magazeti kadhaa, ikilihusisha Gazeti JAMHURI na taarifa hizo.

Bila kuficha, Lake Oil imedai kwamba taarifa hizo (za kukwepa kodi ya Sh bilioni 26) ambazo hazikuitaja Lake Oil, ni za uzushi na zinazolenga kuichafua.

Hata hivyo, JAMHURI bado haijaitaja kampuni hiyo kwa kuwa bado inakamilisha taaarifa zake za kiuchunguzi. Kuibuka kwa Lake Oil kukiri kuwa ndiyo mlengwa, kunachukuliwa kuwa ni msaada mkubwa kwenye uchunguzi wa tukio hilo la ukwepaji kodi ambalo ni la uhujumu uchumi.

Katika ukaguzi uliofanywa katika vituo 30 vya mafuta katika mikoa ya Ruvuma, Njombe na Iringa, vituo kenda, vikiwamo vya Lake Oil, vilifungiwa.

Vituo vingine ni Ahmed Basaleh (Njombe); Ruvuma Oil Supplies – Nanenane Filling Station (Songea), TSN (Songea), Fairtech Investment Filling Station (Mbinga), Oryx (Makambako), Natoil (Mafinga), na Kangesa  (Changarawe) ambacho kwa sasa kinajulikana kama MOGAS.

Kwenye ukaguzi uliofanywa mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro hadi Machi 3, mwaka huu vituo kadhaa vilifungwa.

Vituo hivyo ni Gapco (Singida), Afroil (Kizota), Camel Oil (Miuji), Puma Energy Uhuru Service Station (Dodoma), Oilcom Nassor Filling Station, na gari lililokutwa karibu na Afroil (Kizota) mjini Dodoma.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, alipoulizwa juu ya kufungiwa kwa vituo hivyo, alisema, “Sijapata taarifa rasmi za haya unayoniuliza, lakini suala la ukaguzi wa EWURA kwenye vituo vya mafuta ni la kawaida.

“Ukaguzi ni moja ya mwendelezo wa shughuli za kawaida kabisa za kila siku za EWURA, kama hilo tukio lipo litakuwa siyo kitu kipya kwa EWURA. Nipo Dodoma kikazi, kama ningekuwa ofisini Dar es Salaam ningekuwa na la kusema, kwa sasa sina.”

Kwa kawaida, mafuta yanayouzwa nchini na yale yanayosafirishwa nje ya nchi huwekewa vinasaba kwa lengo la kupambana na udanganyifu kwenye biashara ya mafuta.

Inapobainika kuwa mafuta hayana vinasaba, EWURA hufunga vituo na kutoa taarifa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya watuhumiwa kulipa faini kwa mujibu wa sheria. Faini hiyo kwa sasa ni Sh milioni 7 kwa kila kituo.

By Jamhuri