Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) wameanza kutekeleza Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unoafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira ya Dunia ukiwa na thamani ya shilingi Bilioni 16.8.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu TAFORI Dkt. Revocatus Mushumbusi kwa niaba ya Kamishana wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo Agosti 25, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wataalam wanaohusika katika utekelezaji wa mradi huo.

“Lengo muu la mradi huu unaotekelezwa kwa muda wa miaka mitano ni kukomesha na kubadili mwelekeo mbaya wa uharibifu wa ardhi na upotevu wa bionuwai katika maeneo yaliyoharibiwa ya ukanda wa Misiti ya Miombo Kusini magharibi mwa Tanzania,” alisisitiza Dkt. Mushumbusi.

Mkurugenzi Mkuu TAFORI Dkt. Revocatus Mushumbusi kwa niaba ya kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo akiwasilisha maelezo kwa wataalamu kuhusu mradi wa utekelezaji wa usimamizi shirikishi wa misitu ya Miombo jijini Dodoma.

Akieleza amesema, Mradi utatekelezwa katika ukanda wa Tabora (Kaliua landscape) na Katavi ( Mlele Landscape) ambapo Wizara ya Maliasili kupitia TFS inashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira kupitia Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO).

“Tanzania ni ya pili kwa ukubwa Dunia kwa mtawanyiko wa misitu ya miombo ambapo misitu ya miombo ina asilimia 90 ya misitu mingine. Mwaka 2021- 2022 Mradi ulisainiwa na Mfuko wa Mazingira ya Dunia na FOA Mradi huu unatarajiwa kupunguza uharibifu wa ardhi na upotevu wa Bionuai,” alisisitiza Dkt Mushumbusi.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu TAFORI Dkt. Mushumbusi amesema kuwa mradi utatekelezwa kwa kutumia mbinu shirikishi za usimamizi wa mazingira na unatekelezwa katika nchi 11 ambazo ni Angola, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, Tanzania, Kenya, Burkina faso, Mongolia na Kazakhstan. Kila nchi itapimwa kwa matarajio iliyojiwekea ambapo Tanzania tutapimwa kwa uhifadhi mzuri wa Misitu ya Miombo na namna tulivyoleta tija kwenye mnyororo mzima wa mazao ya nyuki na maisha ya jamii.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS Hussein Msuya amesema kuwa Wakala huo unatambua kuwa uharibifu wa mazingira unadumaza shughuli za kiuchumi, hivyo mradi huu umekuja wakati sahihi.

Aidha, aliwashukuru wajumbe wa kikao hicho cha wataalam watakaohusika katika utekelezaji wa mradi huu kwa namna moja au nyingine na kuwataka kuzingatia kikamilifu mada zitakazowasilishwa katika kikao hicho cha wataalam.

Kamati ya Kikao cha Utekelezaji wa Usimamizi shirikishi wa misitu ya miombo ya nyanda kame wakisikiliza maoni kutoka kwa wajumbe na wataalamu wa mradi huo, jijini Dodoma.

Naye Mwakilishi wa FAO Bw. Charles Tulahi ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano inaotoa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo huu wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame hali inayowezesha kufanikisha uwepo endelevu wa rasilimali misitu na maji.

Aliongeza kuwa FAO imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika utunzaji wa mazingira.

Naye Mwakilishi Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira Bi. Martha Ngalowera amebainisha kuwa Mradi huu utasaidia malengo ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame.

TFS imekuwa ikishairikiana na Wadau wa Maendeleo katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na uhifadhi endelevu wa misitu na hivyo kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu hali itakayochangia katika kukuza uchumi.

By Jamhuri