Balile

Wiki tatu zilizotangulia kabla ya wiki iliyopita, nilichambua kitabu kinachohusu njia mbadala za kufufua uchumi wa Afrika. Nilikisitisha wiki iliyopita tu, kutoa fursa ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Kitabu hiki kinaitwa “Making Africa Work”. Tafsiri isiyo rasmi ya jina la kitabu hiki inamanisha “Mbinu za Afrika Kujikwamua Kiuchumi.” Kitabu hiki kimeandikwa na Greg Mills, Olusegun Obasanjo (Rais mstaafu wa Nigeria), Jeffrey Herbst na Dickie Davis. Kimechapishwa na Taasisi ya Brenthurst Foundation ya Johannesburg, Afrika Kusini. Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ameshiriki uzinduzi wa kitabu hiki katika Hoteli ya New Africa, jijini Dar es Salaam. Nilikuwapo.

Katika sehemu ya kwanza ya mapitio ya kitabu hiki, niliandika kwa kina juu ya ongezeko la watu duniani. Nimeeleza kinachotajwa katika kitabu hiki kwamba Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu milioni 58. Kufikia mwaka 2050 Tanzania itakuwa na watu milioni 138. Afika ina watu bilioni 1.2 kwa sasa. Kufikia mwaka 2050 itakuwa na watu bilioni 2.4 na mwaka 2100 Afrika itakuwa na watu bilioni 5.7. Dunia wakati huo itakuwa na watu bilioni 11, hivyo nusu ya watu duniani watakuwa wanaishi Afrika.

Ni kwa mantiki hiyo nimeona umuhimu wa kitabu hiki na kufanya uchambuzi wa kina juu ya kinachosema kitabu hiki. Niliahidi kuzungumzia madini wiki kabla ya wiki iliyopita, jinsi gani kitabu hiki kinaelekeza. Waandishi wa kitabu hiki wanapendekeza Afrika kuwa na sera zinazotabirika katika sekta ya madini. Wanasema mchakato imara, uliokamilika na sheria zinazotabirika na usimamizi bora ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini.

Wanapendekeza kuangalia mchango wa madini katika uchumi wa taifa si kwa njia ya kodi tu, bali uwepo mtazamo mpana wa kuangalia ajira na masuala mengine. Si hilo tu, wanapendekeza nchi za Afrika kuhakikisha zina umeme wa uhakika na zitambue gharama kubwa za uwekezaji katika migodi au visima vya kuchimba mafuta. Haya yote na mengine yakichanganywa, Serikali na wawekezaji wakakaa meza moja, wanasema nchi za Afrika zitafaidika na wawekezaji nao watafaidika kisha uchumi utakua.

Wanasisitiza kuwa hali ya wananchi na serikali kutowaamini wawekezaji katika sekta ya madini, inavuruga uwekezaji kwa kuwaona wahusika muda wote kuwa ni wezi. Afika ina asilimia 20 ya dhahabu yote duniani, asilimia 23 ya titanium, asilimia 28 ya cobalt, zaidi ya asilimia 60 ya almasi yote duniani, asilimia 80 ya phosphates, asilimia 90 ya chromite na asilimia 96 ya platinum.

Sitanii, kiwango hiki cha madini na mengine mengi ni fursa kwa Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye madini mengi. Hivi karibuni tumebadili sheria zetu za madini kulipa taifa fursa ya kumiliki madini yetu kwa ukamilifu. Baadhi ya nchi zimeanza kuinga hatua tuliyoichukua kama nchi kuhakikisha tunafaidika na hazina hii ya asili.

Kimsingi, nasema hili ni eneo ambalo linaweza kulipatia taifa letu utajiri mkubwa. Kwa muda mrefu madini yamechangia zaidi ya asilimia 12 katika uchumi wa taifa. Tunachopaswa kufanya kama taifa ni kusomesha watu wetu katika sekta hii wakawa na utaalam unaohitajika. Bila kufanya hivyo watakuwa wanakuja wageni na kusomba madini yetu ama kwa kutwambia hayana ubora au kwa kudai wanafanya utafiti na mwisho wa siku tutabaki na mashimo.

Hata hivyo, naomba tusisahau ukweli kwamba kuchimba madini au mafuta kunahitaji mtaji mkubwa. Tutakapokuwa tunajadiliana na wawekezaji, ni vyema tupime kiwango cha faida tunayoilenga na kuwapa wawekezaji fursa ya kuona umuhimu wa kuchimba madini hapa kwetu badala ya kuwakamua hadi wakatususia. Wiki ijayo, usikose sehemu ya 6 ya kitabu hiki inayozungumzia viwanda.

By Jamhuri